Rais Dk. Kikwete azindua Azam Stadium Complex, azitaka klabu nyingine kuiga mfano wa Azam FC

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete leo amezindua kituo cha michezo cha Azam (Azam Stadium Complex), huku akizitaka klabu nyingine nchini kuiga mfano wa Azam FC.

 

Azam Stadium Complex inamilikiwa na klabu ya Azam ambayo ipo chini ya makampuni ya S. S Bakhresa inayomiliki kampuni kadhaa zinazozalisha na kutoa huduma mbalimbali za vinywaji, chakula na usafiri.

 

Akiwa katika sherehe za uzinduzi huo, Dk. Kikwete alitembelea sehemu mbalimbali za kituo hicho ikiwemo viwanja vitatu vya soka, hosteli, bwawa la kuogelea, gym na ukumbi wa kisasa wa kulia chakula.

 

Dk. Kikwete, alisema Azam imeonyesha mfano mzuri kwa kuanzisha kituo hicho ambacho kitatoa fursa kwa vijana wa Tanzania kupata soko la ajira huku soka nchini likisonga mbele.

 

“Nawapongeza kwa mafanikio mliyofikia hadi leo hii, nimesikia katika hotuba yenu kwamba mlianza mwaka 2004 kwa kuunganisha timu za viwanda lakini leo hii mnazisumbua klabu kubwa ambazo zimeanzishwa muda mrefu.

 

“Ninyi ndiyo mtakaoleta maendeleo ya kuinuka kwa soka la Tanzania, kwani hao wengine hawaeleweki wanachokifanya kwani migogoro imetawala katika klabu zao, pia wanaendekeza mambo yasiyofaa katika soka,” alisema Dk. Kikwete.

 

Alisema ana imani Azam itafika mbali kutokana na mipango thabiti iliyojiwekea katika kuhakikisha inainua soka la Tanzania na muda si mrefu itakuwa timu bora Afrika.

 

“Azam imewekeza katika soka kwa kuwa na kituo cha kukuza soka la vijana, hapa watapatikana wachezaji wazuri ambao klabu itawatumia na wengine watauzwa Ulaya. Hii itaifanya Azam kuwa na timu bora wakati wote.

 

“Hichi kinachofanywa na Azam ndicho kinachofanywa na klabu kubwa za Ulaya kama Barcelona ya Hispania ambayo imeweza kuwatoa nyota mbalimbali kama (Cesc) Fabregas na (Lionel) Messi, sasa wanakula matunda ya kile walichopanda,” alisema Dk. Kikwete.

 

Wakati huohuo, kabla Dk. Kikwete hajazungumza, Mkurugenzi wa S. S Bakhresa inayomiliki klabu ya Azam, Abubakar Bakhresa, alisema ujenzi wa kituo hicho umegharimu kiasi cha Sh. 800 milioni na hadi kikikamilika kitakuwa kimetumia jumla ya Sh. 3 bilioni.

 

“Mheshimiwa rais, Azam ilitokana na timu viwanda vitatu vya Azam ambazo zilianzishwa katika mpango maalum wa kulinda afya za wafanyakazi, baadaye ndipo ikapatikana hii timu moja ya Azam mwaka 2004.

 

“Tarehe 21 Julai mwaka 2008, timu hii ilipanda daraja kutoka daraja la kwanza hadi Ligi Kuu na hadi sasa inashiriki ligi hiyo. Ujenzi wa kituo hiki unaendelea na sasa awamu ya kwanza imemalizika na kinachoendelea ni awamu ya pili,” alisema Abubakar.

 

Alisema kwa kutambua mchango wa jamii, shule mbili za jirani na kituo hicho, zimejengewa madarasa, kupewa madawati na kujengewa visima vya maji safi.

 

“Katika kurudisha faida ya kile tunachokipata kutoka kwa jamii, tumezisaidia shule mbili zilizo jirani na kitu hiki, kwa kujenga madarasa, kutoa madawati na kuchimba visima,” alisema Abubakar.

 

Pia Abubakar aliiomba serikali kupunguza au kuondoa kodi ya vifaa vya michezo kwa maendeleo ya michezo nchini. “Tunafanya manunuzi ya vifaa vingi vya michezo, lakini tunakumbana na changamoto kubwa ya kodi, sasa tunaiomba serikali iweze kufikiria upya juu ya hali hii,” alisema Abubakar.

 

Akijibu ombi hilo kupitia hotuba yake, Dk. Kikwete alisema amelisikia ombi hilo na atalifikisha kwa mamlaka zinazohusika lakini alisisitiza pato kubwa la serikali linatokana na kodi