Goli la mchezaji Abdalah Seif ‘Karihe’ wa Azam FC limepeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kupelekea timu hiyo kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Baraack YC II katika mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa ATS jijini Monrovia nchini Liberia.

 

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrka (CAF)  wameshinda mchezo huo wa ugenini katika hatua ya pili ya mashindano hayo makubwa Afrika, mechi ya marejeano itachezwa wiki mbili zijazo jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC wakiwa na kila aina ya sababu ya kushinda kutokana na maandalizi waliyofanya pamoja na mipango mizuri ya timu hiyo iliyowekeza katika soka wameweza kupambana na kupata matokeo hayo na kujiweka vizuri kwa ajili ya kuingia hatua nyingine ya mashindano hayo.

 

Katika mchezo huo Azam FC ilicheza ikimkosa mmoja wa manahodha wake Salum Abubakar ‘Sure Boy’ lakini timu ilicheza vizuri na kuwa na kasi zaidi, mchezaji Kipre Tchetche alikosa magoli mengi ya wazi katika kipindi cha kwanza.

 

BYC walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 44 na kupeleka timu hiyo mapumziko wakiongoza 1-0 dhidi ya Azam FC.

 

Magoli yote ya Azam FC yalipatakana katika kipindi cha pili Humphrey Mieno aliweza kumchezesha kombolela kipa wa BYC na kufunga goli la kusawazisha dk 51 na kufanya matokeo kuwa 1-1.

 

Abdalah Seif ‘Karihe’ aliwainua Watanzania na mashabiki wa Azam FC kwa kuipatia timu hiyo goli la pili katika dakika ya 89 akicheza vizuri krosi iliyopigwa na mchezaji Khamis Mcha na kumaliza mchezo Azam FC wakiondoka na ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji wao BYC II.

Katika mchezo huo Azam FC ilifanya mabadiliko walitoka Ibrahim Mwaipopo dk 69, akaingia Abdi Kassim ‘Babi’, dk 80 aliingia Karihe kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche na dk 85 John Bocco alitoka nafasi yake ikachukuliwa na Jabir Aziz.

Katika mchezo wa jana wachezaji David John Mwantika na golikipa Mwadini Ally walikuwa nyota wa mchezo kwa kucheza vizuri na kuizuia BYC II kupata matokeo ya nyumbani.

Kikosi cha Azam FC kitarejea nchini siku ya Jumanne asubuhi kwa maandalizi ya ligi kuu pamoja na mechi ya marudiano dhidi ya BYC.

 

Azam FC, Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, Daudi Mwantika, Jickins Atudo, Michael Bolou, Tchetche Kipre/Abdalah Seif ‘Karihe’ 80’, Ibrahim Mwaipopo/Abdi Kassim ‘Babi’ 69’, John Bocco/Jabir Aziz 85’, Humphrey Mieno na Khamis Mcha.