Kocha mkuu wa timu ya Azam, Stewart John Hall ameeleza kuwa timu yake itatumia zaidi mbinu ya kushambulia dhidi ya wapinzani wake Barrack Young Controllers II katika mchezo wa raundi ya kwanza wa kombe la Shirikisho utakaopigwa kesho Jumapili mjini hapa.

Kocha Stewart amesema kuwashambulia wapinzani ndiyo itakuwa njia sahihi ya kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza ili hatimaye kujiweka katika mazingira bora ya kufuzu kwa raundi ya pili pale timu mbili hizo zitakaporejeana majuma matatu baadaye jijini Dar es Salaam.

“Tunahitaji goli la ugenini, hilo ndiyo lengo letu la kwanza, hatuwezi kuja hapa na kucheza kwa nia ya kutafuta sare, tutaelekeza mashambulizi ya kutosha kwa wapinzani kwani hatutacheza mchezo wa kujilinda zaidi” alinena  mkufunzi huyo wa raia wa Uingereza.

Azam itakuwa na kumbukumbu nzuri ya kutinga hatua hii ya raundi ya kwanza baada ya kuibamiza Al Nassir ya Sudan Kusini kwa jumla ya magoli 8-1 kutokana na ushindi wa 3-1 nyumbani na 5-0 ugenini mjini Juba.

Kocha Stuwart anasema wachezaji wake wameanza kuelewa umuhimu wa mashindano hasa baada ya kupata ushindi mnono wa ugenini na kucheza vema tofauti na mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ambapo hadi dakika 80 timu zilikuwa zimefungana 1-1.

Kuhusu mazoezi ya timu yake baada ya kuwa mjini hapa kwa siku nne Stewart alisema: “sijaona kitu kipya sana ambacho si cha kawaidatumekuwa vipindi viwili vizuri vya mazoezi tokea tuwasili viwanja viwili ambavyo tumefanyia mazoezi vipo katika hali ya bkufanana na vile tunavyovitumia kule Tanzania kwa hiyo kila jambo limekwenda  vema”

Mkufunzi huyo ameongeza kuwa kutokana na kuwasili mapema anajaribu kutumia ujanja wa kimchezo wakati wa mazoezi kwani anakuwa hana uhakika ni watu gani wanakuwepo kwenya mazoezi yake, japo aliongeza kuwa hilo la watu kuwepo halipi taabu sana kwa amejipanga vilivyo kuwakabili wapinzani kufundi.

Kuhusu hali za wachezaji Stewart amsema: “ Sure (Salum Abubakar hatunaye hapa amebakia Dar es Salaam kutokana na kuwa mgonjwa, kwa hiyo ninao wachezaji 21 hapa, Brian Umony bado hajapona kabisa kwa hiyo hatashiriki katika mchezo huu, hivyo nabakiwa na wachezaji 20 naamini nitapata kikosi imara cha kupata matokeo bora kutoka miongoni mwa hao waliopo.

Alipoulizwa kuhusu wapinzani wa Azam, klabu ya Barrack YC II na kama anafahamu lolote kuhusu uimara na upungufu wao Stewart alisema  amefanikiwa kupata taarifa muhimu kuhusu uwezo wa timu hiyo kiufundi na anaamini taarifa hizo zitakuwa nguzo yake katika kupeleka kilio wa Waliberia.

“Kwaujumla tunafahamu kuwa ni timu ambayo haina uzoefu mkubwa na hivyo haina tofauti sana na Azam, ipo chini ya jopo jipya la uongozi na ambalo linajitahidi kuiimarisha, hata hivyo nakuhakikishia mchezo huu utakuwa ni mzito kwao” alinena kwa kujiamini.

Aliongeza kusema kuwa timu yake haitakuwa na kikwazo cha hali ya hewa kwani si tofauti sana na Dar es Salaam ambayo wachezaji wake wameizoea. Kwa kipindi cha juma lote hili jotoridi limekuwa la wastani wa nyuzijoto 30 ambapo kiwango cha juu ni nyuzijote 35 na kiwango cha chini ni nyuzijoto 25.

Timu ya Azam FC iliyowasili mjini Monrovia Jumatano mchana kwa ndege ya Shirika la ndege la Kenya tayari imefanya mazoezi mara mbili, yaliyofanyika Alhamis jioni katika uwanja unaomilikiwa na klabu ya Barrack YC II itakayoikabli Azam na katika uwanja wa Antoinette Tabman utakaotumika kwa mchezo wa kesho kuanzia saa 10 kimili za hapa sawa na saa moja kamili usiku za Afrika Mashariki. Viwanja vyote viwili ni vya nyasi bandia.

Ujumbe wa watu saba ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Blassy Kiondo na Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrisa uliwasili Monrovia Jumatatu kwa nia ya kufanya matayarisho muhimu kabla ya kuwasili kwa timu.

Ujumbe huo ulifanikiwa kubadili hoteli ya kufikia timu baada ya kubaini kuwa hotel iliyopangwa na wenyeji ya Krystal Ocean View haikukidhi viwango vya Azam FC licha ya klabu mwenyeji na chama cha mpira wa miguu cha Liberia (LFA) kusistiza kuwa goteli hiyo imepishwa na CAF na FIFA baada ya ukaguzi na kwamba timu mblaimbali za klabu na za taifa zimekuwa zikifikia hapo bila ya malalamiko yoyote.

Hivyo timu ipo katika hotel ya Golden Key iliyopo jirani na Uwanja wa Taifa uitwao Samuel Kanyon Doe (SKD) wenye uwezo wa kubeba watazamaji 35,000, uliojengwa wakati wa utawala wa Rais Samuel Doe ambaye aliuawa na majeshi ya waasi mwaka 1990.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza kati ya Azam na Barrack YC II utachezeshwa na waamuzi kutoka Misri ambao ni Farouk Mohamed, Abou Elela Ahmed, Abou Elsada Tamer na Younis Yasser. Kamishna wa mchezo ni Adama Samba kutoka Gambia.

Iwapo Azam itafanikiwa kuitoa BYC II itapambana na mshindi kati ya FAR Rabat ya Morroco na Al Nassri ya Libya ambazo zinapambana leo Jumamosi mjini Rabat.