Timu ya Azam FC imetoka sare ya 1-1 na Polisi Moro katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Matokeo hayo yamezigawanyisha timu zote pointi moja moja, Azam FC imefikisha pointi 37, nyuma ya Yanga inayoongoza kwa kuwa na pointi 45.

 

Katika mchezo huo Azam FC walimtumia kipa wao namba mbili Aishi Salum aliyeweza kuhimili mchezo huo na kuokoa mikwaju ya hatari iliyokuwa ikipigwa na wachezaji wa Polisi Moro.

 

Azam FC walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 5 kupitia kwa mshambuliaji John Bocco aliyepiga mpira wa adhabu baada ya mabeki wa Polisi kumtendea madhambi Humphrey Mieno wa Azam FC nje ya eneo la penati.

 

Matokeo hayo yalidumu hadi kumalizika kipindi cha kwanza Azam FC wakiongoza kwa 1-0, kipindi cha pili kilianza kwa kasi Polisi wakiwa na kila aina ya jitihada za kusaka bao la kusawazisha.

 

Dakika ya 53 kosa la beki wa Azam FC, David Mwantika kunawa mpira katika mstari eneo la hatari uliwapatia penati timu ya Polisi iliyomriwa na mwamuzi Simon Mbelwa, Polisi hawakufanya makosa baada ya mchezaji Lambow Mauli kupiga vizuri penati hiyo na kubadili matokeo kuwa 1-1.

 

Azam FC walifanya mabadiliko kuimarisha kikosi chake walitoka Jabir Aziz dk 61 akaingia Michael Bolou, dk 72 katoka John Bocco nafasi yake ikachukuliwa vyema na Abdi Kassim ‘Babi’ na dk 82 aliingia Uhuru Selemani kuchukua nafasi ya Khamis Mcha.

 

Mabadiliko hayo hayakubadilisha matokeo na kufanya timu zote kutoka sare ya 1-1, sare hiyo imewapunguzia kazi Polisi na kuwapa ahueni kwa kuwa wanahitaji pointi nyingi kuhakikisha wanabaki katika ligi kuu.

Katika mchezo huo dk ya 90 mwamuzi Mbelwa alimtoa kwa kadi nyekundu beki David Mwantika wa Azam FC baada ya kumuonyesha kadi mbili za njano.

Azam FC, Aishi Salum, Waziri Salum, David Mwantika, Malika Ndeule, Luckson Kakolaki, Jabir Aziz/Michael Bolou 61’, Salum Abubakar, Humphrey Mieno, John Bocco/Abdi Kassim ‘Babi’ 72’, Kipre Tchetche na Mcha Khamis/Uhuru Seleman 82’.