Ushindi wa 5-0 dhidi ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini, umeipa Azam FC nafasi ya kuingia hatua ya pili ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa timu hiyo kwa jumla ya magoli 8-1.

Azam FC inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imefanikiwa kuvuka hatua ya awali na kuingia hatua ya pili ambapo zimesalia timu 36.

Azam FC imefikisha idadi hiyo ya magoli baada ya kupata ushindi wa 3-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita na leo wakacheza mechi ya pili kwenye Uwanja wa Juba nchini Sudan Kusini na kupata ushindi mnono wa 5-0 wakiwa ugenini na kufikisha jumla ya magoli 8-1.

Kwa timu za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya CAF, ni Azam FC pekee iliyosalia baada ya timu za Simba SC kutolewa na Recreativo Libolo ya Angola kwa jumla ya magoli 5-0, na Jamhuri ya Pemba nayo ikatolewa na St. George ya Ethiopia kwa kipigo cha jumla cha 8-0 zote zilikuwa zinacheza Klabu Bingwa Afrika.

Azam FC wanabaki kuwa wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya CAF, watakutana na mshindi kati ya Barrack Y. C. II ya Liberia na Johansens ya Sierra Leone.

Katika mchezo wa leo ambao Azam FC walipata ushindi wa 5-0, magoli yalifungwa na Khamis Mcha magoli matatu ‘Hat Trick’, John Bocco na Salum Abubakar wamefunga goli moja moja.

Azam Fc katika mchezo wake wa kwanza ilipata ushindi wa 3-1 magoli ya Azam FC yakifungwa na Abdi Kassim na Kipre Tchetche aliyefunga magoli mawili.

Kikosi kamili cha Azam Fc kitarejea nchini kesho kwa maandalizi ya mchezo wao mwingine wa Kombe la Shirikisho utakaochezwa kati ya Machi 15-17 mwaka huu.