MECHI namba 120 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Februari 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam imeingiza sh. 239,686,000.

Pichani juu wachezaji wa Azam FC wakimlalamikia mwamuzi baada ya kukataa goli lililoonekana halali lililofungwa na John Bocco

Kiasi hicho cha pesa ni kikubwa na rekodi kwa vilabu nje ya Simba na Yanga zinapocheza pamoja. licha ya kupatikana kwa kiasi hicho cha pesa, kwa mara nyingine tena tatizo la kumalizika kwa tiketi na mfumo mbovu wa uuzwaji wa tiketi ulijitokeza ambapo maelfu ya mashabiki walilazimika kurejea makwao baada ya kukosa tiketi za kuingilia uwanjani

Watazamaji 39,315 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 58,794,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 36,562,271.19.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 33,315 na kuingiza sh. 165,655,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 485 na kuingiza sh. 9,700,000. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 29,895,725.82, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 17,937,435.49, Kamati ya Ligi sh. 17,937,435.49, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 8,968,717.75 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 6,975,669.36.