Mshambuliaji John Bocco amerejea kwenye ligi kuu akifunga goli moja huku timu yake Azam FC ikiendeleza ushindi wake wa nne mfulilizo baada ya kuichapa JKT Ruvu 4-0 katika mchezo wa VPL uliochezwa uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

Pichani juu, John Bocco katka mechi dhidi ya Al Nassir Juba, Picha kutoka Blogu ya Bin Zubeiry

 

Bocco alikuwa nje ya uwanja kwa takriban miezi miwili, amerejea kwenye ligi kuu baada ya kukosa michezo mitatu, mshambuliaji huyo amerudi na kasi yake ile ile na kutuma salamu kwa timu watakazokutana nazo.

 

Matokeo ya mchezo huo yameifikisha Azam FC kuwa na pointi 36 sawa na Yanga lakini Yanga bado ana mchezo mmoja ambao watacheza dhidi ya Azam FC Jumamosi hii.

 

Katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu, Azam FC ilicheza ikiwakosa wachezaji wake Brian Umony, Michael Bolou, Uhuru Seleman wanaosumbuliwa na majeraha pamoja na kiungo mchezeshaji Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyetumikia adhabu kwa kuwa na kadi za njano tatu.

 

Azam FC inayoundwa na wachezaji mahiri walianza kulisakama lango la JKT Ruvu mapema katika dakika ya pili ya mchezo ambapo mchezaji mwenye kasi Khamis Mcha alipiga shuti likatinga moja kwa moja wavuni na kuandika bao la kwanza kwa Azam FC.

 

JKT Ruvu wakaanza kulipa mashambulizi, dakika ya 10 wakapata penati baada ya  kipa Mwadini Ally wa Azam FC kumtendea madhambi Amosi Mgisa, penati hiyo ilimriwa na mwamuzi Israel Nkongo wa Dar es Salaam.

 

Mchezaji Kisimba Luambano atabeba lawama zote kwa kukosa penati hiyo, mchezaji huyo alipiga penati ikachezwa vizuri na kipa Mwadini na kurejea uwanjani na kuokolewa na wachezaji wa Azam FC matokeo yakawa Azam FC 1-0 JKT Ruvu.

 

Azam FC walitandaza soka kama kawaida, Bocco alitumia vema dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza kwa kuandika bao la pili akicheza vizuri pasi ya Humphrey Mieno na kupiga shuti likatinga wavuni, Mieno aliweza kumpiga chenga kipa wa JKT Ruvu, Shaaban Dihile na kutoa pasi hiyo iliyomfikia Bocco, timu zikaenda mapumziko Azam FC wakiwa mbele kwa 2-0.

 

Kipindi cha pili kilianza wakati JKT Ruvu wakianza kujipanga, dk 46 Mcha akawafunga goli la tatu kwa shuti la mbali lililompita kipa Dihile wa JKT na kumuweka chini asijue la kufanya na kuiacha Azam FC ikiongoza 3-0.

 

Baada ya ushindi huo kocha Stewart Hall aliwapeleka mapumziko dk 67 Kipre Tchetche aliyefanya kazi nzuri nafasi yake ikachukuliwa na Abdalah Seif ‘Karihe’ aliyeingie kuongeza kasi ya mchezo, dk 71 Bocco alirudi benchi baada ya kufunga goli moja akaingia mtaalam Abdi Kassim ‘Babi’.

 

Mabadiliko hayo yaliichanganya JKT Ruvu, wakiwa wanajipanga kuwakabili Babi na Karihe, Badi aliwapachika bao la nne katika dakika 73 akiunganisha mpira uliopigwa na Jabir Aziz, Babi akatulia na kumchenga kipa Dihile na kuachia shuti lililotinga wavuni na kubadilisha matokeo kuwa Azam FC 4-0 JKT Ruvu.

 

Baada ya matokeo hayo JKT Ruvu walifanya mabadiliko walitoka Kisimba Luambano, Amos Mgisa na Mussa Hasan ‘Mgosi’ nafasi zao zikachukuliwa na Hussein Dumba, Emmanuel Pius na Ally Khamis, mabadiliko hayo hayakuweza kubadilisha matokeo ya mchezo huo uliomalizika Azam FC kuibuka na ushindi wa 4-0.

 

Katika mchezo huo dk 44 Mcha alipiga shuti likagonga mwamba na kurudi uwanja huku dk 84 Seif Karihe na Jabir Aziz walipiga mashuti ya mbali yakagonga mwamba na kutoka nje hizo ni nafasi chache walizokosa wachezaji wa Azam FC.

 

Huu ni ushindi wa nne mfululizo kwa Azam FC, walianza mzunguko huu wa pili kwa kuwafunga Kagera Sugar na Toto Africa 3-1 kila mmoja, wakaifunga Mtibwa Sugar 4-1 wakiwa ugenini Manungu Complex, Turiani mkoani Morogoro na leo wameichapa 4-0 JKT Ruvu.

 

Azam FC watacheza mechi ya tano dhidi ya Yanga siku ya Jumamosi, mechi inayohitaji ushindi ili waongoze ligi na kujiweka vizuri kusaka taji la ligi kuu msimu huu wa 2012/2013.

 

Akizungumzia matokeo ya 4-0 dhidi ya JKT Ruvu, kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema ni sehemu ya mafanikio kwa wachezaji wake, walitakiwa kupata magoli mengi zaidi, pia ni salamu kwa timu walibakisha.

 

“Nimefurahi kupata pointi tatu zikiwa na magoli mengi tangu tuanze mzunguko huu washambuliaji wangu wamejitahidi, tumeshinda kuanzia goli tatu, ni mwanzo mzuri na tutaendelea nao, sasa tunajiandaa kuikabili Yanga” alisema kocha huyo kutoka nchini Uingereza.

 

Azam FC: Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Jockins Atudo, Jabir Aziz, Tchetche Kipre/Abdalah Seif ‘Karihe’ 67’, Ibrahim Mwaipopo/Gaudence Mwaikimba 81’, John Bocco/Abdi Kassim ‘Babi’ 71’, Humphrey Mieno na Khamis Mcha.

 

JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Mussa Zuber, Kessy Mapande, Kisimba Luambano, Dismas Makwaya, Jimmy Shoji, Amos Mgisa/Emmanuel Pius, Nashon Naftari, Samwel Kamtu, Mussa Hasan ‘Mgosi’/Ally Khamis na Hussein Bunu.