Magoli ya wachezaji Abdi Kassim ‘Babi’ na Tchetche Kipre wa Azam FC, yameipa ushindi wa 3-1 timu hiyo dhidi ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini na kuiweka katika nafasi nzuri kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pichani juu, Nahodha wa Azam FC John Bocco akimtoka beki wa Al Nassir Juba, Picha kwa husani ya blogu ya Bin Zubeiry

Azam FC wametumia vema uwanja wao wa nyumbani, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakiwa mbele ya maelfu ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia timu hiyo ikiondoka na ushindi mnono katika mchezo wake wa kwanza wa mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

 

Kijituma na umahiri wa wachezaji wa Azam FC katika mchezo huo umechangia kupatikana kwa matokeo hayo mazuri, safari ya kusaka ushindi ilianza mapema, katika dakika ya 14 Abdi Kassim ‘Babi’ alitumia vema nafasi iliyoipata na kuandika bao la kwanza kwa Azam FC, Azam FC 1-0 Al Nasri Juba.

 

Azam FC ilipata pigo katika mechi hiyo baada ya mshambuliaji wake aliyekuwa anawatesa mabeki wa Al Nasri, Brian Umony kuumizwa na kushindwa kuendelea na mchezo katika dk 15 na nafasi yake ikachukuliwa Khamis Mcha aliyeitendea haki nafasi hiyo muda wote wa mchezo.

 

Kiungo ambaye alikuwa nahodha wa timu Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliwakamata vilivyo sehemu ya katikati na kufanya anavyotaka kwa kutengeneza mashambulizi mengi hali iliyowapa shida mabeki na kipa wa Al Nasri Juba.

 

Dk 35 Al Nasri waliamua kumtendea madhambi Michael Bolou wa Azam FC kwa lengo la kumzuia lakini akaumia na kushindwa kuendelea na mchezo, Bolou alirejea benchi nafasi yake akaingia Jabir Azizi kuendeleza kasi.

 

Wakiwa wameonekana kujisahau walinzi wa Azam FC walishindwa kumzui mchezaji Fobian Elias wa Al Nasri na kusawazisha goli hilo katika dakika ya 38, goli hilo lilidumu hadi mapumziko timu zikilitoka zikiwa sare ya 1-1.

 

Kipindi cha pili Azam FC waliingia wakiwa na kasi mpya muda wote walikuwa wakicheza soka la hali ya juu na kuwahamisha timu nzima ya Al Nasri kuanza kulinda goli lao, Babi dk 47 alipiga mpira ukatoka nje na dk 54 Azam FC walifanya shambulizi Kipre alipiga shuti likagonga mwamba na kurudi ndani, mpira ukatua miguu kwa Jabir Azizi naye akapiga shuti likatoka nje mita chache karibu na lango la Al Nasri.

 

Kasi hiyo iliongezeka zaidi katika dakika 69 alipoingia mshambuliaji John Bocco kuchukua nafasi ya Babi aliyefunga goli la kwanza, kuingia kwa Bocco kulipokelewa kwa furaha na mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo.

 

Bocco dk 70 alijaribu kufunga akapiga mpira ukaokolewa na beki wa Al Nasri, Miskin Emannuel, wachezaji wa Azam FC waliongeza kasi kadri muda unavyokwenda, dk 80 Tchetche Kipre akaipatia Azam FC bao la pili kwa kichwa akimalizia kazi nzuri iliyotengenezwa na Khamis Mcha, na kufanya matokeo kuwa 2-1.

 

Azam FC wakawa kama wameamshwa, Sure Boy aliendelea kumiliki mpira na kuonekana karaha kwa wachezaji wa Al Nasri waliokuwa wanapitwa muda wote, Humphrey Mieno alikosa nafasi nyingi za wazi, akatumia nafasi aliyoipata dk 90 kumpatia Tchetche krosi iliyozaa bao la tatu, Tchetche alifunga goli hilo kwa kichwa na kuamsha mashabiki waliokuwa wanaishangilia Azam FC, kwa kubadilisha matokeo na kuwa 3-1 Al Nasri Juba.

 

Mchezo ukamalizika Azam FC wakipata ushindi mnono wa 3-1 dhidi ya Al Nasri, wakisubiri mechi ya marejeano itakayochezwa wiki mbili zijazo nchini Sudan Kusini.

 

Wachezaji wameonekana na furaha kubwa wakishangilia, kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema ushindi huo ni mwanzo, wamemaliza mechi hiyo wanaelekeza kwenye mchezo wa marejeano.

“Tumaliza kwa ushindi wa 3-1, sisi kwetu ni kama mwanzo, nawataka wachezaji wangu wasibweteke zaidi waongeze nguvu kwenye maandalizi ya mchezo ujao, kwa kuwa tutakwenda Sudan kushinda”alisema kocha Hall.

 

Azam FC: Mwadini Ally (GK), Himid Mao, Malika Ndeule, David Mwantika, Jockins Atudo, Michael Bolou/Jabir Aziz 35’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Humphrey Mieno, Brian Umony/Khamis Mcha ‘Vialli’ 15’, Abdi Kassim ‘Babi’/John Bocco 69’ma Tchetche Kipre.

 

Sub: Aishi Salum, Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Abdulhalim Humud, Seif Abdalah ‘Karihe’, Gaudence Mwaikimba, Seleman Uhuru na Omari Mtaki

Benchi la ufundi: Kocha Stewart Hall, msaidizi Ibrahim Shikanda, kocha wa makipa Idd Abubakar, Daktari Mwanandi Mwankemwa na Paul Gomez

 

Al Nasri: Peter Midia, Joseph Odongo, Miskin Emmanuel, Abdalah Sebit, Simon Amanya, Johson James/Adnan Nan 67’, Abdalmelik Sebit/Emmanuel Manas 79’, Ladu Manas, Kon James, Jacob Osuru na Fobian Elias.