Wiki mbili kabla ya kucheza mechi za kimataifa za Shirikisho la Soka Afrika, wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano hayo Azam FC imewafunga wawakilishi wenzao Simba SC 3-1 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo asubuhi, uwanja wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Simba SC inashiriki mashindano hayo upande wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika huku Azam FC wao watacheza kombe la Shirikisho Afrika, mechi zitakazoanza rasmi Februari 15-17 mwaka huu, Azam FC wataanza na Al Nasri Juba ya Sudan Kusini huku Simba wao watacheza na Clube Rec. Libolo ya Angola.

 

Katika mchezo huo wa kujipima timu zote zilipanga wachezaji ambao hawajapata nafasi katika vikosi vya kwanza vya timu hizo tangu kuanza  kwa mzunguko wa pili wa ligi inayoendelea ya 2012/2013.

 

Simba walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa Edward Christopher dk 18 aliyepiga mpira wa juu ukazama moja kwa moja wavuni na kumpita kipa wa Azam FC, Jackson Wandwi.

 

Azam FC walipata magoli yote matatu katika kipindi cha pili ambapo goli la kusawazisha lilipatikana dk 64 kupitia kwa Ibrahim Mwaipopo aliyefunga kwa kichwa akimalizia mpira uliopigwa na nahodha wa mchezo huo Himid Mao.

 

Dk 66 Seif Abdalah Karihe aliandika bao la pili kwa Azam FC kwa shuti baada ya kupokea krosi ya Kipre Tchetche na kumpita kipa wa Simba Abuu Hashim na kufunga goli hilo.

 

Karihe alikuwa mwenye bahati kutokana na soka safi lililochezwa muda huo, Azam FC wakapata goli la tatu kupitia kwa Karihe aliyecheza vizuri mpira uliopigwa na Michael Bolou baada ya kuwapita mabeki wa Simba na kufunga goli hilo ambalo lilimaliza mchezo Azam FC ikipata ushindi wa 3-1 dhidi ya Simba SC.

Kabla ya mechi hiyo ilitangulia mechi kati ya Azam Academy ambao walitoka suluhu na Simba B.

Timu zote mbili zimeshacheza mechi mbili za ligi kuu, Simba walishinda mchezo wa kwanza 3-1 dhidi ya African Lyon na wakatoka sare ya 1-1 katika mechi ya pili walipokutana na JKT Ruvu.

 

Azam FC imeshinda michezo yote miwili ya mzunguko wa pili kwa kuzichapa Kagera Sugar na Toto Africa 3-1 kila mmoja mechi zilizopigwa uwanja wa Azam Complex Chamazi .

 

Jumamosi Azam FC itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoni Morogoro, huku Simba wao watakuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kucheza dhidi ya JKT Oljoro.

 

Azam FC, Jackson Wandwi, Himid Mao, Haji Nuhu/Mlika Ndeule, Luckson Kakolaki, Omari Mtaki/ David Mwantika, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Kipre Tchetche/Mchael Bolou, Gaudence Mwaikimba/ Uhuru Seleman na Abdalah Seif Karihe.