Siku chache kabla ya kucheza mechi za Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa Azam FC yupo katika maandalizi ya kuelekea nchini Sudan Kusini kuangalia mechi chache za wapinzani wao timu ya Al Nasri Juba.

 

Mechi hiyo ya hatua ya awali za mashindano ya kombe hilo, Azam FC wataanza wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es Salaam wiki mbili zijazo.

 

Akizungumza na www.azamfc.co.tzleo asubuhi kocha Stewart amesema amewasilisha ombi la kutaka kwenda kuiona timu hiyo na viongozi wanafatilia utaratibu ili akaione timu hiyo ikicheza mechi zake za ligi kabla kabla ya mechi yao ya Shirikisho.

 

Amesema dhumuni la kuiona timu hiyo ni kujua aina ya mchezo wanaocheza ili aandae kikosi chake vizuri na kuwajenga wachezaji wake kulingana na mchezo wa timu hiyo ya Sudan Kusini.

 

“Nimepanga kwenda Sudan hivi karibuni, kucheza bila kumjua mpinzani wako inakuwa ngumu, nitatumia muda huo kuwajua wapinzani wetu ili kupata picha ya mchezo utakavyokuwa pamoja na kuiandaa timu yangu” amesema Stewart.

 

Ameongeza kuwa kwa sasa timu ipo katika maandalizi makali kwa ajili ya mechi hiyo ambayo wanacheza kwa mara ya kwanza, pamoja na mchezo wao wa ligi kuu utakaochezwa Feb 9 mwaka huu dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

 

 

Dk. Mwankemwa: Bocco kurudi uwanjani wiki nne zijazo

 

Mshambuliaji John Bocco wa Azam FC anatarajiwa kurejea uwanjani rasmi wiki nne zijazo baada ya kusumbuliwa na mejeraha ya mguu kwa zaidi ya mwezi mmoja.

 

Bocco aliumia akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ Desemba mwaka jana ilipokuwa ikishiriki mashindano ya Kombe la Chalenge 2012, aliporejea jijini, klabu yake ya Azam FC ikampeleka nchini India kwa matibabu zaidi na kurejea nchi wiki mbili zilizopita.

 

Akizungumzia hali ya mchezaji huyo, daktari wa Azam FC, Dk. Mwanandi Mwankemwa amesema kwa sasa anaendelea vizuri ameanza mazoezi na maumivu yemeanza kupungua hali inayomfanya kuanza vizuri mazoezi hayo madogo madogo.

 

“Bocco anaendelea vizuri, hali yake inaimarika siku baada ya siku, hadi kufikia wiki nne zijazo atakuwa yupo vizuri kuanza kucheza kwa sasa anafanya mazoezi ya taratibu akiwa chini ya uangalizi wa daktari” alisema Dk. Mwankemwa.

 

Dk. Mwankemwa amesema mazoezi anayofanya Bocco yatamsaidia kurudi katika hali yake ya kawaida mapema pamoja na kutibu tatizo hilo kwa kuwa kupata matibabu sahihi kwa mchezaji kunamjenga na kumfanya apone na kuendelea kucheza.