Magoli ya wachezaji wa kimataifa wa Azam FC, Brian Umony, Michael Bolou na Humphrey Mieno (Pichani Juuyameipatia ushindi wa 3-1 timu hiyo dhidi ya Toto Africans, katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC wanapata ushindi wao wa pili katika mzunguko huu wa pili na kufikisha pointi 30 ikiwa nyuma ya Yanga yenye pointi 32 huku Simba wakiwa watatu wana pointi 26.

 

Katika mchezo wa leo wachezaji hao pamoja na timu nzima walionyesha mpira mzuri muda wote wa mchezo na kuipeleka puta timu ya Toto.

 

Azam FC walianza kalamu hiyo ya magoli mapema katika dakika ya 4 ya mchezo kupitia kwa mchezaji Michael Bolou aliyepiga mpira uliompita kipa wa Toto, Nelson Kimati na kutinga moja kwa moja wavuni.

 

Goli hilo liliwachanganya Toto, huku upande wa Azam FC walifanya mashambulizi na kupatikana goli la pili dakika ya 13 lililowekwa wavuni na mshambuliaji Brian Umony na kuwa goli lake la kwanza kufunga katika ligi kuu akiwa na Azam FC.

 

Baada ya kupatikana kwa magoli hayo Azam FC walianza kucheza soka wanavyotaka na kuonyesha uwezo wao huku wakiisumbua mara kwa mara ngome ya Toto.

 

Nahodha wa Azam FC, Salum Aboubakar aliingoza vyema timu hiyo sehemu ya kiungo akiwa pamoja na Bolou, Mieno na Khamis Mcha, David Mwantika, Haji Nuhu, Jockins Atudo na Malika Ndeule walisimama vizuri sehemu ya ulinsi huku Abdi Kassim akisaidiana na Umony waliitendea haki safu ya ushambuliaji.

Azam FC walifanya mabadiliko dk 77 alitoka Bolou nafasi yake ikachukuliwa na Abdulhalim Humud na dk 82 Gaudence Mwaikimba aliingia kuchukua nafasi ya Mieno, mabadiliko hayo yalifanyika kutokana na rafu walizokuwa wanacheza wachezaji wa Toto.

Toto hawakuwa nyuma kipindi cha kwanza walifanya mashambulizi mchezaji Kheri Mohamed akiwa yeye na kipa Mwadini Ally wa Azam FC alishindwa kufunga na kupiga mpira uliotoka nje, kukosa magoli kulimfanya kocha wa Toto, John Tegete kufanya mabadiliko ya kwanza dakika ya 29 alitoka Uluere Chika nafasi yake ikachukuliwa na Seleman Kibuta, mabadiliko yalimaliza kipindi cha kwanza Azam FC wakiwa mbele kwa 2-0 dhidi ya Toto.

 

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi, Azam FC waliandika goli la tatu kupitia kwa kiungo Humprey Mieno aliyefunga kwa kumalizia mpira alitengenezewa na Umony matokeo yakawa 3-0.

 

Toto walipata goli lao la pekee katika dakika ya 73 baada ya mabeki wa Azam FC kujichanganya na kumuacha mchezaji Seleman Kibuta kumpita kipa wa Azam FC, Mwadini na kupiga mpira uliosindikizwa na mabeki Jockins Atudo na David Mwantika wakitaka kuokoa bao hilo, goli hilo lilimaliza mchezo Azam FC ikipata ushindi wa 3-1 dhidi ya Toto.

 

Baada ya mchezo huo kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema matokeo hayo ni mazuri kwake na kwa timu nzima, amewapongeza wachezaji kwa kucheza vizuri.

Amesema kilichopo sasa watafanya maandalizi kwa ajili ijayo dhidi ya Mtibwa Sugar, akiizungumzia mechi hiyo Stewart amesema itakuwa mechi ngumu.

 

“Ni mechi yetu ya ugenini tunaenda kucheza, tunahitaji kujiandaa zaidi pia tunatakiwa kushinda” alisema Stewart.

 

Azam FC itacheza mechi yake ya 16 ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar, Februari 9, Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

 

Azam FC, Mwadini Ally, Malika Ndeule, Samih Haji Nuhu, David Mwantika, Jockins Atudo, Michael Bolou/Abdulhalim Humud 77’, Brian Umony, Salum Abubakar ,Sure Boy’, Abdi Kassim ‘Babi’, Humphrey Mieno/Gaudence Mwaikimba 82’ na Khamis Mcha.

 

Nelson Kimati, Erick Muliro, Robert Magadula, Erick Kyaluzi, Everist Maganga, Peter Mutabuzi, Severin Costantine, Donald Obimma, Uluere Chika, Kheri Mohamed na Mohamed Jingo.