Timu ya Azam FC imeanza vema mzunguko wa pili wa ligi kuu kwa kuifunga Kagera Sugar 3-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC wakiwa na wachezaji wapya waliowasajili walicheza katika kiwango cha juu na kupelekea kupata ushindi huo ulioingezea timu hiyo pointi tatu na kufikisha pointi 27 katika msimamo wa ligi kuu ya Tanzania VPL.

 

Katika mchezo huo Azam FC walianza kwa kushambulia mapema katika dakika ya 5 Abdi Kassim ‘Babi’ alipopiga shuti likatoka nje mita chache, Babi alirekebisha makosa yake na kuipatia Azam FC bao la kwanza dk 18 kwa shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

 

Goli hilo la kwanza liliamsha kasi ya mashambulizi na kujiamini kwa wachezaji wa Azam FC ambao walionekana kuonana muda wote wa machezo, huku wachezaji wapya beki David Mwantika, Brian Umony kutoka Kenya na Jockins Atudo na Humphrey Mieno waliomudu vyema  nafasi zao na kuongeza kasi ya mchezo.

 

Azam FC hawakucheza mbali na lango la Kagera Sugar, dakika ya 29 Khamisi Mcha alipngeza bao la pili kwa Azam FC akitumia vema krosi ya Brian Umony aliyemtoka beki wa Kagera, Salum Kanoni na kupiga mpira uliomfikia Mcha na kuandika goli hilo la pili.

 

Kagera nao walijitahidi kufanya mashambulizi katika kipindi hicho cha kwanza dk 22 mchezaji Juma Mpola alipiga shuti likaokolewa na kipa wa Azam FC, Mwadini Ally na dk 24 Daudi Jumanne alipiga mpira akiwa yeye na lango la Azam FC lakini akapiga mpira ukatoka nje na kuifanya Azam FC ikiongoza 2-0 Kagera katika kipindi cha kwanza.

 

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Kagera wakisaka nafasi ya kusawazisha magoli hayo huku Azam FC wao wakisaka nafasi ya kuongeza goli jingine dk ya 69 Mcha aliipatia Azam FC goli la tatu akicheza vizuri krosi ya kichwa iliyopigwa na Babi, Mcha alifunga goli hilo kwa shuti lililompita kipa Andrew Ntalia wa Kagera Sugar.

 

Azam FC walifanya mabadiliko kwa kuwapumzisha wachezaji wake wa kimataifa, Michael Bolou dk 67 na kuingia Ibrahim Mwaipopo, dk 75 alitoka Umony akaingia Seif Abdalah ‘Karihe’ na dk 79 aliingia Jabir Aziz kuchukua nafasi ya Humphrey Mieno.

 

Goli la Kagera Sugar lilipatikana baada ya mabadiliko, walitoka Juma Mpola dk 58 na Daudi Jumanne 63 nafasi zao zikachukuliwa na Paul Ngwai na Themi Felix, Ngwai aliipatia Kagera goli la kufutia machozi dk 81 akitumia uzembe wa beki ya Azam FC, na kupelekea kumalizika mchezoo huo Azam FC ikitoka na ushindi wa 3-1.

 

Matokeo hayo yanaipa Azam FC ushindi wa pointi sita kutoka kwa timu ya Kagera baada ya mechi ya kwanza kuifunga 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

 

Azam FC itaingia kambini kwa maandalizi kwa ajili ya mchezo wake wa pili utakaokuwa dhidi ya Toto Africa.

 

Kocha wa Azam FC amefurahishwa na viwango vya wachezaji wote, hasa wapya waliosajiliwa dirisha dogo na kusema mechi zijazo zitakuwa nzuri na timu itapata ushindi.

 

“Tumewakosa Kipre Tchetche na John Bocco, lakini timu imecheza vizuri, wachezaji wapya wameendelea kufanya vizuri, kazi iliyopo ni kushinda michezo ijayo” alisema Kocha Stewart.

 

Kikosi Azam FC: Mwadini Ally, Malika Ndeule, Samih Haji Nuhu, David Mwantika, Jockins Atudo, Michael Bolou/Ibrahim Mwaipopo 67’, Brian Umony/Seif Abdalah 75, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Humphrey Mieno/Jabir Aziz 79 na Khamis Mcha.

 

Kagera: Andrew Ntalia, Benjamin Asukile, Salum Kanon, Benjamin Effe, Amandus Nesta, George Kavila, Julius Mrope, Juma Nade, Shija Mkina, Daudi Jumanne/Them Felix 63’ na Juma Mpola/Paul Ngwai 58