AZAM FC imeondoka leo na wachezaji 22 na viongozi sita kuelekea Nairobi Kenya kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya pazia la ligi kuu mzunguko wa pili kufunguliwa.

Katika msafara huo wachezaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’, Waziri Salum na Kipre Herman Tchetche, wameachwa katika safari ya klabu yao hiyo nchini Kenya kutokana na majeruhi.

Azam imeondoka leo Alfajiri kwenda Nairobi kwa kutumia usafiri wa basi lake la kisasa kwa ziara ya wiki moja ya kucheza mechi za kujipima nguvu kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakiwa nchini Kenya Azam FC watacheza na Sofapaka, AFC Leopards na timu nyingine ambayo wenyeji wetu watatupangia alisema kocha mkuu wa Azam FC Stewart Hall ambaye ndiye aliyehusika kuandaa ziara hiyo.

Mabingwa hao wa Mapinduzi Cup misimu miwili mfululizo wanaendelea kucheza michezo mingi ya kirafiki ili kuwasaidia wachezaji wapya kuweza kuelewa mfumo wa uchezaji wa Azam FC, wachezaji wapya kwenye kikosi cha Azam FC ni beki kisiki David Mwantika, kiungo Humphrey Mieno, na washamburiaji Seif Rashid Karihe, Uhuru Selemani na Brian Umony

Tayari Azam FC ilipata mechi tano nchini DRC na kutwaa kombe na Ngao ya Hisani, ikapata mechi tano tena na kutwaa kombe la Mapinduzi na inaelekea Kenya kupata mechi tatu za majaribio na kufanya jumla ya mechi 13

Katika mechi kumi ilizocheza, Azam FC imeshinda michezo sita, imetoka sare michezo mitatu na kupoteza mmoja tuu dhidi ya Dragons ya DRC