Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi Azam FC ikiwa pungufu usiku huu imefanikiwa kutinga fainali za mashindano hayo baada ya kuifunga Simba SC kwa penati 5-4 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa.

 

Mchezo huo uliomalizika kwa mikwaju ya penati, mchezaji wa Azam FC Malika Ndeule alipiga penati ya ushindi hiyo huku Haruna Athumani wa Simba akikosa penati na kuiacha Azam FC ikishinda katika mchezo huo uliomaliza dakika 120 zikiwa sare ya 2-2.

 

Hii ni mara ya pili kwa Azam FC kuitoa Simba katika nusu fainali ya Mashindano hayo, mwaka jana Azam FC iliifunga Simba 2-0 katika nusu fainali uliyochezwa uwanja huo.

 

Penati za Azam FC ziliwekwa wavuni na Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Jockins Atudo, Haji Nuhu na Malika Ndeule upande wa Simba zilifungwa na Miraji Madenge, Jonas Mkude, Miraji Adam na Ramadhan Kipendamoto.

 

Baada ya matokeo hayo Azam FC inasubiri kucheza na mshindi wa mechi ya kesho usiku kati ya Tusker FC ya Kenya na Miembeni utakaochezwa katika uwanja huo.

 

Katika mchezo huo Azam FC walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 9 kupitia kwa mchezaji Humphrey Mieno aliyefunga kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyopigwa na Ibrahim Mwaipopo.

Wachezaji wa Azam FC walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa goli moja bila dhidi ya Simba, mchezo huo ulisimama kwa dakika nne katika kipindi hicho baada ya umeme kukatika uwanjani, ulikatika dk 14-19 uliendelea tena.

 

Kipindi cha pili Simba walisawazisha bao hilo katika dakika ya 77 kupitia kwa mchezaji Rashid Ismail aliyepiga shuti la mbali lililokwenda moja kwa moja wavuni, goli la pili lilifungwa dakika ya 109 na mchezaji Miraji Madenge aliyetumia ujanja wa kuuweka mpira vizuri kwa mkono bila kuonawa na mwamuzi.

Timu zote zilifanya mabadiliko upande wa Simba waliingia Emily Mgeta, Isihaka Hassan, Miraji Madenge, Said Demla kuchukua nafasi za Ramadhan Singano, Abdalah Seseme, Marcel Kacheza na Athmani Hassan Khatibu.

 

Azam FC walifanya mabadiliko walitoka Seif Abdalah, Brian Umony na Humphrey Mieno nafasi zao zilichukuliwa na Gaudence Mwaikimba, Jabir Aziz na Malika ndeule.

 

Katika mchezo huo mwamuzi aliwatoa kwa kadi nyekundu wachezaji wawili wa Azam FC Ibrahim Mwaipopo dk 108 alionyeshwa kadi mbili za njano na Jabir Aziz alimtendea madhambi Emily Mgeta wa Simba katika dakika ya 115.

 

Dk 119 mchezaji Atudo aliisawazishia Azam FC pungufu kwa mkwaju wa penati iliyoamriwa na mwamuzi Sheha baada ya beki wa Simba Emily Mgeta kumwangusha Malika katika eneo la hatari, na kupelekea matokeo ya 2-2.

 

Azam FC Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Atudo, Michael Bolou, Seif Abdala/Mwaikimba, Ibrahim Mwaipopo (red 108’), Brian Umony/Malika Ndeule, Humphrey Mieno/Jabir Aziz (red 115’).

 

Simba William Mweta, Miraji Adam, Paul Ngalema, Hassan Hatibu, Komabil Keita, Jonas Mkude, Ramadhan Singano/Miraji Madenge, Abdalah Seseme/Said demla, Marcel Kacheza na Haruna Athman.