Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi Azam FC leo usiku wamefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano hayo ambapo watakutana na Simba SC,katika nusu fainali itakayochezwa siku ya Alhamis, Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Azam FC imetinga hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kumaliza mchezo wa mwisho ikitoka suluhu na Mtibwa Sugar na kufikisha pointi 5, katika mchezo mwingine Miembeni nayo ilifanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kutoka suluhu na Coastal Union.

Kwa matokeo hayo Mtibwa Sugar na Coastal Union zimeaga mashindano hayo, Coastal imemaliza ikiwa na pointi tatu imetoka sare michezo yote mitatu huku Mtibwa wamemaliza na pointi mbili baada ya kufungwa mchezo mmoja na kutoka sare michezo miwili.

Azam FC itakutana na Simba kwa mara nyingine katika mchezo wa nusu fainali za mashindano hayo ambapo mwaka jana 2012 timu hizo zilikutana na Azam FC ikaibuka na ushindi wa 2-0, nusu fainali ya kwanza itachezwa Jumatano kati ya Tusker FC ya Kenya dhidi ya Miembeni FC.

Katika mchezo wa leo kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar, timu zote zilianza kwa kasi ya kutafuta goli, Mtibwa Sugar waliingia kusaka ushindi wa zaidi ya goli 5-0 ili waweze kufuzu wakati Azam FC walihitaji matokeo aina yoyote kuweza kuingia hatua hiyo.

Kipindi cha kwanza kila timu ilifanya mashambulizi Mtibwa walibadilisha aina ya mchezo tofauti na michezo miwili iliyopita walicheza kwa kasi lakini utengenezaji wa nafasi ilikuwa mdogo.

Azam FC waliutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi, wachezaji wake wapya wa kimataifa Brian Umony, Humphrey Mieno na Jockins Atudo walicheza katika kiwango kinachotakiwa na kuleta upinzani katika mchezo huo ambapo mshambuliaji Gaudence Mwaikimba alikosa nafasi mbili za wazi kwa kupiga mipira nje akiwa yeye na lango la Mtibwa.

Kipindi cha pili timu zote ziliingia uwanja na kucheza kwa kushambuliana, Azam FC walifanya mabadiliko walitoka Khamis Mcha dk 46 akaingia Uhuru Seleman, dk  62 alitoka Mieno akaingia Ibrahim Mwaipopo na dk 68 aliingia Abdalah Seif kuchukua nafasi ya Umony, mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mashambulizi lakini hayakubadili matokea na kupelekea mpira kumalizika timu zote zikiwa zimetoshana nguvu kwa sare ya bila kufungana.

Azam FCMwadini Aally, Himid Mao, Samih Haji Nuhu, David Mwantika, Jockins Atudo, Michael Bolou/Jabir Aziz 88’, Brian Umony/Abdala Seif 68’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Gaudence Mwaikimba, Humphrey Mieno/Ibrahim Mwaipopo 62’ na Khamis Mcha/ Uhuru Seleman 46’.

Mtibwa Hussein Sharif, Khamis Issa, Yusuf Nguya, Rajab Mohamed, Salvatory Ntebe, Babu Ally Seif/Masoud Ally, Vincent Barnabas/Juma Mkopi,Rashid Gumbo, Hussein Javu, Juma Luizio na Ally Mohamed/Juma Mpakala 89’.

 

Msimamo wa mwisho Kundi B

                                    P     W     D      L     GF   GA   GD    Pts

Azam FC                     3      1      2       0      3       1      2       5

Miembeni FC               3      1      1       1      5       4      1       4

Costal Union                3      0      3       0      1       1      0       3

Mtibwa Sugar               3      0      2       1      2       5     -3      2