Mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC wamejiweka katika nafasi nzuri ya kuingia nusu fainali ya mashindano hayo baada ya kuifunga Miembeni FC 3-1 katika mchezo uliochezwa leo usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Brian Umony pichani juu akiruka mkwanja wa Adeyum SalehPicha kwa hisani ya Blogu ya Binzubeiry

Azam FC imepata ushindi huo muhimu na kuongoza kundi hilo ‘B’ kwa kuwa na pointi nne, ikifuatiwa na Miembeni yenye pointi 3, Coastal Union ina pointi mbili huku Mtibwa wakiwa wa mwisho kwa kuwa na pointi 1.

Katika mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa ulianza kwa kasi na dakika ya pili Azam FC walipata bao la kwanza lililofungwa na beki aliyesajiliwa hivi karibuni Jockins Atudo aliyefunga kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyochongwa vyema na kiungo Humphrey Mieno wote kutoka Kenya.

Miembeni walisawazisha goli hilo dakika mbili baadaye, kupitia kwa mchezaji Adeyum Ahmed aliyepiga mpira wa kona ambao mwamuzi aliona ulioenda moja kwa moja wavuni.

Kupatikana kwa goli hilo kuliurudisha mchezo huo kuwa wa kasi na kushambuliana zaidi huku wachezaji wa Azam FC, Mieno,  David Mwantika, Brian Umony na Khamis Mcha walicheza vizuri kwa kuonana na kutengeneza nafasi nyingi.

Safu ya ulinzi ilisimamiwa vizuri na nahodha Himidi Mao, Atudo, Samih Haji Nuhu na Mwantika, tangu muda huo waliweza kuzui mashambulizi ya Miembeni na kuwapa nafasi washambuliaji wa Azam FC kupanda juu na kutengeneza nafasi.

Mshambulia mrefu na mwenye nguvu Gaudence Mwaikimba aliipatia Azam FC goli la pili baada ya kuunganisha mpira uliopigwa na Mieno na kuwapita mabeki wa Miembieni na kupiga shuti lililotinga moja kwa moja wavuni, goli hilo lilizipeleka timu hizo mapumziko Azam FC wakiwa mbele kwa 2-1.

Kipindi cha pili kilianza na sura mpya, timu zote ziliwakosa walimu wake Stewart Hall wa Azam FC na Salum Bausi wa Miembeni baada ya kutolewa na mwamuzi wa mchezo huo Ally Kisaka baada ya kumzonga mwamuzi huyo wakati wa mapumziko.

Azam FC ilifanya mabadiliko kuimarisha kikosi chake walitoka Mcha dk 60 nafasi yake ikachukuliwa na Uhuru Selemani, dk 65 aliingia Seif Abdalah kuchukua nafasi ya Umony, dk ya 82 walitoka Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Mieno nafasi zao zikachukuliwa na Jabir Aziz na Ibrahim Mwaipopo.

Mabadiliko hayo yaliongeza nguvu kwa Azam FC na kuinyanyasa ngome ya Miembeni, dk 87 Uhuru aliipatia Azam FC goli la tatu kwa shuti baada ya beki wa Miembeni kuokoa shuti la Mwaikimba, mpira ukarudi uwanjani ndipo Uhuru alitumia nafasi hiyo kuwainua mashabiki wa Azam FC na kumaliza mchezo Azam FC ikipata ushindi huo wa 3-1.

Kwa matokeo hayo Azam FC imejiweka katika nafasi nzuri ya kuingia nusu fainali ya mashindano hayo ambayo mustakabali wake utaamliwa kwenye mechi za Jumatatu ambazo Azam FC itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar huku Coastal Union wakimenyana na Miembeni mshindi katika mechi hizo ataingia nusu fainali.

Kocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amesema matokeo hayo mazuri kwa timu wamebakisha kibarua cha kuitoa Mtibwa Sugar ili wavuke na kuingia nusu fainali.

Alisema wataingia katika maandalizi kesho kwa kuwa wanaijua timu hiyo hivyo haitawasumbua sana kuliko kukutana na timu ambazo hawajawahi kucheza nazo.

Azam FC, Mwadini Ally, Himid Mao, Samih Haji Nuhu, David Mwantika, Jockins Atudo, Michael Bolou, Brian Umony/Seif Abdalah 60’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ /Jabir Aziz 82’, Gaudence Mwaikimba, Humphrey Mieno/ Ibrahim Mwaipopo 82’ na Khamis Mcha/Uhuru Seleman 65.

Miembeni, Seleman Hamad, Mfaume Odela, Adeyum Saleh, Salum Haji, Salum Juma, Sabri Ally, Laurent Mugiya, Seleman Haji, Monja Liseki/ Mohamed Salum, Rashid Roshua/Peter Ilunda na Issa Othman.