AZAM FC leo imefanikiwa kutinga nusu fainali mbili kwa mpigo, ile ya Kombe la Uhai kwa vijana wa Under 20 na  Kombe la Hisani mjini kinshasa, baada ya kuilaza Real de Kinshasa kwenye Uwanja wa Martyrs, katika mchezo maalum wa kutafuta timu ya kutinga Nusu ya michuano hiyo inayoandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka DRC.
 
Shukrani kwao, washambuliaji Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi.
Ikiongezewa nguvu na nyota wake watatu, Kipre Tchetche, Kipre Balou raia wa Ivory Coast na Mkenya, Joackins Atudo waliochelewa mechi mbili za awali, Azam leo ilitawala mchezo na kama si rafu za wapinzani wao, ingevuna ushindi mtamu.
 
Hadi mapumziko, tayari Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na Mwaikimba dakika ya 21, ambaye aliunganisha pasi nzuri ya Kipre kutoka wingi ya kushoto.
 
Hilo linakuwa bao la pili kwa Mwaikimba, mshambuliaji wa zamani wa Kahama United, Ashanti United, Yanga, Prisons na Kagera Sugar katika mechi tatu za mashindano haya alizocheza, awali alifunga katika sare ya 1-1 na Dragons.
Kipre Tchetche alilazimika kutoka nje ya Uwanja dakika ya 43 kutokana na rafu za wachezaji wa Real, nafasi yake ikichukuliwa na Samih Hajji Nuhu.
 
Real walikuwa wakipiga kiatu haswa na kiungo Waziri Salum aliungana na Kipre Tchetche kuuacha Uwanja kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo, ingawa nafasi yake ilichukuliwa na Uhuru Suleiman dakika ya kwanza ya kipindi cha pili.
Awali ya hapo, refa Madila Achille alimtoa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43 beki Muipalayi Igongo kwa kumchezea rafu mbaya Gaudence Mwaikimba, ambayo chupuchupu naye imtoe nje, kiasi  cha kulazimika kumalizia mechi akichechemea.
 
Kipindi cha pili, Azam waliendelea kuwafundisha soka Real na katika dakika ya 73, kazi nzuri ya Mwaikimba ilisaidia kupatikana bao la pili. Mpira mrefu uliopigwa na kipa Mwadini Ally, Mwaikimba aliumiliki vema, akatoa pasi pembeni kushoto kwa Hajji Nuhu ambaye aliingia ndani kidogo na kukata krosi maridadi iliyounganishwa kimiani na Seif.
Humphrey Mieno alikuwa mwathirika mwingine wa rafu za Real, baada ya kulazimika kutoka nje dakika ya 77, akimpisha Abdi Kassim ‘Babbi’.
 
Azam walionekana kuridhika baada ya kuwa wanaongoza mabao 2-0 na wakafanya uzembe uliowapa bao la kufutia machozi Real, lililofungwa na Bisole Panzu dakika ya 78.
 
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall aliwapongeza vijana wake, lakini akasema anakabiliwa na wakati mgumu katika hatua inayofuata kutokana na wachezaji wake wanne kuumia leo.
 
Kocha wa Real, Sandra Makombele aliwasifu Azam ni timu nzuri na akasema anakubali matokeo, ingawa aliwapiga kijembe. “Wachezaji wangu wana mazoezi mengi, Azam hawana mazeozi, wakiguswa kidogo wanaumia, hakukuwa na rafu, ule ni mchezo wa nguvu kama Ulaya, kocha wao inabidi awape mazoezi mengi wawe wagumu,”alisema mwanamama huyo.
 
Katika mechi zake mbili za awali za Kundi B, Azam ilitoka 1-1 na Dragons na ikafungwa 2-0 na Shark FC.
Azam ilicheza mechi zote mbili bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na Msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
 
Watano hao, waliwasili mjini Kinshasa jana na beki Joackins Atudo naye amewasili leo na wote wameshiriiki mchezo wa leo kikamilifu.
 
Nusu Fainali zitachezwa Desemba 25 wakati Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu. 
Kikosi cha Azam leo kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum/Uhuru Suleiman dk46, Omar Mtaki/Joackins Atudo dk46, David Mwantika, Jabir Aziz, Kipre Balou/Malika Ndeule dk85, Seif Abdallah, Kipre Tchetche/Samih Hajji dk43, Humphrey Mieno/Abdi Kassim dk77 na Gaudence Mwaikimba.
 
Katika Mashindano ya Uhai Cup
 
TIMU za Azam Academy na Mtibwa Sugar zimekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu) kuzamisha African Lyon mabao 3-1. na JKT Ruvu 1-0
 
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam,  hadi mapumziko Mtibwa Sugar ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 22 na Hillary Kasela. Hassan Kabunda aliisawazishia African Lyon katika dakika ya 53.
 
Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Godfrey Mohamed dakika ya 64 na Juma Lazio akapachika la mwisho dakika ya 87. Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar sasa itacheza mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Azam ambayo nayo leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu) iliilaza JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Chamazi. Bao la Azam lilifungwa dakika ya 46 na Mudathiri Yahya.
 
Mechi hiyo ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Nusu fainali ya pili nayo itachezwa kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10 kamili jioni.
 
Robo fainali ya tatu kati ya Oljoro JKT na Simba, na robo fainali ya nne zinachezwa leo saa 10 kamili jioni (Desemba 19 mwaka huu) kwenye viwanja vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.