Muda mchache kabla ya kuanza kwa mashindano ya kuwania kombe la vijana U20 kwa vilabu vya ligi kuu (Uhai Cup 2012), Azam Academy amejipanga kuhakikisha wanatwaa kombe hilo kwa mara nyingine.

 

Michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa itakutanisha timu zote 14 zinazoshiriki ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2012/2013, itaanza kesho Desemba 12-23 mwaka huu kwenye viwanja vya Kumbukumbu ya Karume na Azam Stadium Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na toviti ya www.azamfc.co.tz kocha msaidizi wa Azam Academy, Iddi Cheche amesema kikosi hicho kimejiandaa na kipo tayari kushindana na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

 

“Mwaka huu tumejiandaa vizuri, timu iko imara kwa maandalizi ya kutosha tofauti na mwaka jana, tunauhakika wa kutwaa ubingwa japo mashindano yatakuwa magumu” alisema kocha Cheche.

 

Aliongeza kuwa wameziba mapengo yalijitokeza katika mashindano yaliyopita kwa kuwapa mafunzo zaidi vijana wao ili kwenda sawa na mashindano hayo.

Azam Academy itaanza mechi yake ya kwanza kesho jioni katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi dhidi ya JKT Mgambo ya Tanga.

 

Katika mashindano hayo timu hizo zimegawanyika makundi ambapo kundi A linaundwa na timu za Coastal Union, JKT Ruvu, Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons na Toto Africans, Kundi B lina African Lyon, Azam, Mgambo Shooting, Polisi Morogoro na Simba, wakati timu za Kagera Sugar, Oljoro JKT, Ruvu Shooting na Yanga zinaunda kundi C.

 

Mechi za ufunguzi zitachezwa kesho African Lyon vs Polisi Morogoro (asubuhi Chamazi), uwanja wa Karume asubuhi, Coastal Union vs Tanzania Prisons na jioni JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar huku Jumatano Kagera Sugar itacheza na Oljoro JKT (Karume) na Yanga dhidi ya Ruvu Shooting (Azam Complex).  

 

Kombe la Uhai lilianzishwa mwaka 2008, ambako Azam Academy ilitwaa kombe hilo mwaka 2009 na 2009, 2010 kombe hilo likachukuliwa na Ruvu Shooting na mwaka jana lilienda kwa Simba B.