MWENYEKITI wa klabu ya Azam FC, Mhe; Abubakar Bakhresa pamoja na bodi ya wakurugenzi wa Azam FC na SSB, wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa aliyekuwa msanii maarufu wa muziki na filamu, Hussein Ramadhani Mkiety, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, kilichotokea jana usiku mkoani Tanga.

Hussein alikuwa na ukaribu na Management ya SSB akifanya matangazo mbalimbali ya bidhaa zinazotengenezwa na SSB kama Azam Cola ambalo alishirikiana na King Majuto.

Kwa niaba ya klabu ya Azam FC  na kwa niaba ya SSB, Mwenyekiti anapenda kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu kutokana na msiba huu mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la Tanzania.

Sharo Milionea ni kijana wa mfano katika jamii ya Tanzania kwani aliamua kutafuta kipato chake kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na mwenyezi mungu ambacho ni uchekeshaji na baadaye kujiingiza kwenye matangazo ya promosheni ya redio na TV pamoja na kuimba muziki wa kizazi kipya.

Mola na ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Hussein Ramadhani Mkeity