Timu ya Azam FC imeendeleza ubabe kwa timu za ligi kuu baada ya kuifunga Polisi Moro 1-0 kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro.

Azam FC imepata ushindi huo wa ugenini na kuwa imeshinda michezo minne mfululizo ikifikisha pointi 16, kwa kushinda michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja.

Ushindi wa leo umeipa Azam FC rekodi ya kucheza michezo mitano ya VPL bila wavu wake kutikiswa huku golikipa Mwadini Alli akiweka kwenye vitabu vya kumbukumbu rekodi ya kusimama langoni mechi nne bila kuruhusu goli.

Rekodi nyingine ni ya kipre Tchetche ya kufunga magoli manne idadi inayomfanya abakize magoli mawili tuu kufikia rekodi ya mwaka jana ambapo msimu mzima alifunga magoli sita pekee.

Katika mchezo huo timu zote zilicheza kwa hari ya kutafuta ushindi, Azam FC wakitengeneza nafasi nyingi.

Kipindi cha kwanza dk 5 mshambuliaji John Bocco alijaribu kutaka kufunga lakini akashindwa kumalizia krosi ya Salum Abubakar 'Sure Boy' na kupiga mpira uliotoka nje.

Pia kipindi hicho Kipre Tchetche alipiga mpra wa kichwa uliotoka nje dk 7, dk 16 na 28 Bocco naye alipiga mipira iliyotoka nje akiwa amebaki yeye na golikipa wa Polisi Moro..

Japokuwa uwanja haukua katika kiwango kizuri, kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kasi kila moja ikihitaji ushindi.

Dk 63 Kipre Tchetche aliifungia Azam FC bao la kwanza na pekee katika mchezo huo akitumia vema uzembe wa kipa wa Polisi Moro Manzi Manzi aliyepangua shuti la Bocco na kuanza kuuchezea mpira ndipo Kipre alipouchukua na kupiga shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.

Goli hilo lilidumu hadi mpira ulipomalizika, Polisi watajutia nafasi walizopata dk 18 Faustine Lukoo na dk 72 Iman Mapunda walipiga mipira iliyookolewa na kipa Mwadini Ally wa Azam FC, huku dk 90 Malimi Basungu alianguka mwenyewe golini na kushindwa kufunga.

Mabadiliko Azam FC walitoka Himid Mao dk 78, Abdulhalim Humud dk 84 na Kipre Tchetche dk 89 baada ya kufanya kazi nzuri, nafasi zao zikachukuliwa na Michael Bolou, Abdi Kassim na Gaudence Mwaikimba.

Kocha wa Azam FC, Boris Bunjak 'Boca' amefurahishwa na ushindi huo na kuahidi kuendeleza ushindi huo katika mechi zijazo.