Mshambuliaji John Bocco wa Azam FC ameipatia timu hiyo pointi tatu baada ya kuifunga African Lyon 1-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifikisha Azam FC katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa sawa na Simba SC zikitofautiana idadi ya magoli.

Azam FC katika mchezo huo ilionyesha nia ya kutafuta ushindi mapema katika kipindi cha kwanza ambapo dakika ya 22 Bocco akiwa na kipa Abdul Seif wa Lyon alipiga shuti lililookolewa na kipa huyo.

Bocco hakukata tamaa na kujaribu kufunga mara kadhaa ndipo dakika ya 44 akaipatia Azam FC goli akitumia vema kosa la kipa Seif wa Lyon aliyepangua shuti la Kipre Tchetche na mpira kurudi uwanjani ndipo Bocco alipotumia nafasi hiyo kwa kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Kiungo anayekuja kwa kasi Himid Mao akishirikiana na viungo wenzake Ibrahim Mwaipopo, Abdi Kassim ‘Babi’ na Jabir Aziz walimudu vizuri nafasi zao kwa kutengeneza mashambulizi na kuharibu mipango ya Lyon.

Golikipa Mwadini Ally amedhihirisha umuhimu wake wa kukaa golini kwa kuokoa mashuti ya wachezaji Benedict Jacob na Hood Mayanja wa Lyon akisaidiwa na mabeki wake Agrey Moris, Erasto Nyoni, Said Morad na Samih Haji Nuhu.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko Lyon waliingia Idd Mbaga dk 66 na Paul Kidande awachezaji hao waliongeza kasi ya mashambulizi lakini hawakubadilisha matokeo ya mchezo huo.

Azam FC nao hawakusita waliwapeleka benchi Ibrahim Mwaipopo dk 63, Himid Mao dk 65 na Tchectche Kipre dk 81 nafasi zao zikachukuliwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Abdulhalim Humud na Gaudence Mwaikimba.

Mchezaji wa Azam FC, Samih Haji alitolewa nje kwa kadi nyekundu dk 87 baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano na mwamuzi Israel Nkongo, Haji alimwangusha Jacob Masawe dk 79 na dk 86 akagongana na Idd Mbaga.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha wa Azam FC, Boris Bunjak ‘Boca’ alisema amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake na matokeo ya kutofungwa hata mchezo mmoja.

Alisema kutofungwa katika michezo mitano ni faraja kwake hivyo anatazamia kuweza kushinda katika michezo yake ijayo ili kuiweka timu yake katika nafasi nzuri ya kusaka kombe la ligi kuu.

“Kwangu ushindi ni faraja, haijalishi ni magoli mangapi bali kupata pointi ni kitu muhimu, tumeshinda na kutoka sare sasa tunajiandaa zaidi kuhakikisha tunashinda michezo ijayo” alisema kocha huyo.

Azam FC katikati ya wiki ijayo itasafiri hadi mkoani Morogoro kucheza dhidi ya Polisi Moro, baada ya mchezo huo timu itaelekea mkoani Mbeya kucheza Tanzania Prisons.

Kikosi Azam FC,  Mwadini Ally, Agrey Moris, Erasto Nyoni, Said Morad, Samih Haji Nuhu(redcard 87), Ibrahim Mwaipopo Salum Abubakar  63’/, Abdi Kassim ‘Babi’,  Jabir Aziz, Himid Mao/Abdulhalim Humud 65’, Tchetche Kipre/ Mwaikimba 81’ na John Bocco.