Licha ya kutoshuka dimbani katikati ya wiki hii, Azam FC ina uhakika wa kusalia katika nafasi ya pili na kama itaporomoka basi ni kwa nafasi moja tuu hadi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu ingawa timu nne zinazoshika nafasi tano za juu kwenye msimamo wa ligi kuu VPL zinashuka dimbani.
Simba SC inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 12 itakwaana na Yanga yenye pointi saba huku JKT Oljoro ikiikaribisha Coastal Union ya Tanga, zote zina point inane.
Matokeo ya Sare baina ya watani wa jadi hayatabadili nafasi ya Azam dhidi ya Simba na Yanga zaidi yataiweka Azam FC kwenye nafasi nzuri ya kukwea kileleni itakapokwaana na African Lyon wikiendi hii.
Sare itamaanisha Simba kufikisha pointi 13 huku yanga ikifikisha point inane. Tayari Azam FC ina pointi 10 na itakuwa na mchezo mkononi.
Kwa upande wa wagosi wa kaya na maafande wa JKT Oljoro, matokeo ya sare yatamaanisha kila timu kufikisha pointi tisa na kuiacha Azam FC ikijidai kwenye nafasi ya pili licha ya kutoshuka dimbani na kama matokeo yatakuwa tofauti na hivyo, timu itakayoshinda itaipiku Azam FC kwa pointi moja.
Ikiwa Yanga itataka kuipiku Azam FC kwenye nafasi ya pili basi italazimika kuifunga Simba zaidi ya wastani wa magoli matatu kitu ambacho kitaashiria simba kupoteza usukani wa ligi kwa Azam FC endapo Azam FC itaifunga African Lyon wikiendi hii.
Azam FC inaendelea na maandalizi yake ikijiwinda na mpambano dhidi ya African Lyon kwenye uwanja wake wa nyumbani mchezo ambao utafuatiwa na safari ya Morogoro na nyanda za juu kusini (Green City Mbeya) kukwaana na timu ngumu ya Tanzania Prisons.
Ligi kuu ya Vodacom wikiendi hii ilinoga kutokana na mechi zake kuoneshwa live na kituo bora cha TV cha kulipia cha Supersport 9 East katika wiki iliyopewa jina la Super Sunday.