Timu ya Azam FC imejiongezea pointi tatu baada ya kuifunga JKT Ruvu 3-0 katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Matokeo hayo yameipeleka Azam FC kileleni kwa msimamo wa ligi kuu ikiwa na jumla ya pointi 10, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 9 kabla ya mchezo wao wa leo Jumamosi dhidi ya Jeshi la Magereza Mbeya.

 

Azam FC waliingia uwanjani katika mchezo huo wakiwa na hali ya ushindi wakitafuta pointi hizo tatu muhimu.

 

Safari ya ushindi ilianza dakika ya 7 ya mchezo ambapo mshambuliaji John Bocco alipiga mpira ukaokolewa na kipa Shaban Dihile wa JKT Ruvu, Kipre Tchetche dakika ya 9 alipiga shuti likatoka nje.

 

Azam FC waliongeza mashambulizi pamoja na kucheza vizuri hasa eneo la kiungo lililokuwa chini ya Abdi Kassim huku mchezaji Himid Mao akitawala muda wote wa mchezo, Jabir Aziz na Ibrahimu Mwaipopo walizimudu vyema nafasi zao na kuiweka timu hiyo katika hali ya ushindani.

 

Dakika ya 45 Mshambuliaji John Bocco aliipatia Azam FC bao la kwanza kwa mkwaju wa penati iliyoamuliwa na mwamuzi Amon Paul wa Mara baada ya beki wa JKT Ruvu, Stanley Nkomola kumwangusha mchezaji huyo kwenye eneo la hatari.

 

Timu zilienda mapumziko Azam FC ikiwa mbele kwa 1-0 dhidi ya JKT Ruvu, kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi JKT Ruvu walifanya mabadiliko walitoka Damas Makwaya na Furaha Tembo nafasi zao zikachukuliwa na Hasan Kikutwa na Haruna Adolf.

 

JKT wakifanya mabadiliko hayo Azam FC kabla ya kufanya mabadiliko walipata goli la pili lililowekwa wavuni kwa kichwa na mshambuliaji kutoka Ivory Coast Tchetche Kipre katika dakika ya 66 akimalizia mpira wa mwisho uliopigwa na Samir Haji Nuhu.

 

Kipre amefikisha idadi ya magoli matatu katika mechi nne alizocheza akifuatiwa na Abdulhalim Humud mwenye magoli mawili huku John Bocco, na Bolou Kipre wameifungia Azam FC goli moja moja.

 

Wakiongoza 2-0 Azam FC iliwapumzisha Abdi Kassim dk 67 nafasi yake ikachukuliwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, dk 79 alitoka Mwaipopo aliyefanya kazi nzuri uwanjani nafasi yake ikachuliwa na Bolou Kipre.

 

Mabadiliko hayo yaliimarisha safu ya kiungo ya Azam FC na kutengeneza mashambulizi mengi ambapo akitokea benchi Bolou alipeleka furaha klabuni kwake kwa kufunga goli la tatu na la mwisho katika mchezo huo akiunganisha krosi kutoka kwa nduguye Kipre Tchetche.

 

Safu ya ulinzi ya Azam FC ikiwa chini ya nahodha Agrey Morris, Erasto Nyoni, Samir Haji Nuhu, na Said Morad waliweza kuwazui washambuliaji wa JKT Ruvu, Azam FC ilimtoa John Bocco nafasi yake ikachukuliwa na Gaudence Mwaikimba katika dakika ya 85.

 

Golikipa Mwadini Ally alikuwa sehemu ya ushindi huo kwa kuzuia mashambulizi ya wachezaji Husein Bunu dk 38 na 60, Furaha Tembo na Ally Khan, huku wachezaji Credo Mwaipopo na Haruna Adolf wakiikosesha JKT ushindi kwa kupiga mipra iliyotoka nje.

 

Azam FC walicheza mchezo huo ambao ni wa kwanza kuonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Super Sport katika mechi tano za ligi kuu zilizopata nafasi ya kuonekana katika kituo hicho.

 

Kikosi cha Azam FC kitaingia katika maandalizi maalum kwa ajili ya mechi yake ya tano dhidi ya Africa Lyon itakayochezwa Octoba 7, kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

 

Azam FC, Mwadini Ally, Agrey Morris, Erasto Nyoni, Samih Haji Nuhu, Said Morad, Himid Mao, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo/Bolou Kipre 79’, Abdi Kassim’Babi’/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ 67’, Tchetche Kipre na John Bocco/Gaudence Mwaikimba 85’.

 

JKT Ruvu Shaaban Bihile, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Hussein Dumba, Damas Makwaya, Ally Khan, William Sylvester, Jimmy Shoji, Hussein Bunu, Furaha Tembo na Credo Mwaipopo.