Timu ya Azam FC imetoka sare ya 2-2 na Toto Africans katika mchezo wa pili wa ligi kuu ya Tanzania uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Azam FC imemaliza michezo miwili ya Kanda ya Ziwa kwa kuondoka na pointi nne, baada ya kushinda mchezo wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar na kutoka sare na Toto Africans.

Katika mchezo huo Toto walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika 20 ya mchezo kupitia kwa Seleman Kiduta, Azam FC ilisawazisha goli hilo dakika ya 26 kupitia kwa kiungo Abdulhalim Humud ambaye tunaweza kusema alikuwa nyota wa mchezo huo.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu zote kwenda mapumziko zikiwa sare ya 1-1, kipindi cha pili Azam FC waliingia uwanjani wakiwa na kasi na kutengeneza nafasi nyingi.

Dakika ya 83 Kipre Tchetche aliunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Abdi Kassim na kuipatia Azam FC bao la pili lakini halikudumu ambapo dakika za nyongeza Evarist Maganga wa Toto alisawazisha bao hilo kutokana na uzembe mkubwa wa kipa Deo Munishi Dida na mchezo kumalizika timu hizo zikigawana pointi moja moja kwa kutoka sare ya 2-2.

Wachezaji wa Azam FC, Ibrahim Mwaipopo alikosa nafasi za wazi baada ya kupiga mipira iliyotoka nje na mlinzi Erasto Nyoni alipiga shuti likangonga mwamba katika dakika ya 42 ya mchezo.

Azam FC walifanya mabadiliko alitoka Jabir Aziz nafasi yake ikachukuliwa na mchezaji chipukizi Hhimid Mao, mabadiliko hayo yalimarisha sehemu ya kiungo ya timu hiyo.

Kikosi hicho kilisharejea jijini Dar es Salaam kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wao wa tatu wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Sept 22, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi .

 Azam FC Deogratius Munishi, Erasto Nyoni, Ibrahim Shikanda, Aggrey Mmoris, Said Morad, Abdulhalim Humud, Ibrahim Mwaipopo, Jabir  Aziz/Himid Mao, John Bocco, Tchetche Kipre na Abdi Kassim ‘Babi’.