Kiungo Abdulhalim Humud wa Azam FC ameianzishia vyema timu yake safari ya ligi kuu msimu wa 2012-2012 kwa kuifungia goli pekee katika mchezo ambao timu hiyo imepata ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Azam FC imeshinda mchezo huo wa ugenini uliochezwa kwenye uwanja mgumu wa Kaitaba mkoani Kagera na kujipatia pointi hizo tatu muhimu ikiwa ligi  imeanza rasmi leo.

Timu hiyo imekabiliana na changamoto nyingi kubwa ikiwemo ni hali ya hewa  ambako mkoa wa Kagera kuna baridi kuliko Dar es Salaam ambapo  Azam FC wanafanya mazoezi yao ya kila siku.

Akizungumza na www.azamfc.co.tz kutoka mkoani Kagera, kocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amesema mchezo ulikuwa mgumu kwa kuwa Kagera walijiandaa vizuri.

"Kucheza ugenini mechi ya kwanza huwa ni ngumu, na hasa ukicheza na Kagera Sugar mechi inakuwa ngumu zaidi, nashukuru jitihada za wachezaji zimetupatia ushindi, ni furaha kwetu hii ni mara ya kwanza tunaifunga Kagera kwao" alisema Kali.

Kali aliongeza kuwa kujitolea kwa wachezaji wake na kupigana dakika zote za mchezo zimechangia kiasi kikubwa kupatikana kwa ushindi huo ukizingatia timu imecheza katika mazingira tofauti.

Kocha huyo amewataka wachezaji wake waongeze juhudi, wajitume na kujitolea zaidi katika mechi zote ili kufikia matarajio yao.

Azam FC kesho itaelekea mkoani Mwanza kwa ndege tayari kwa maandalizi ya kucheza na Toto Africans kwenye mchezo wake wa pili wa ligi kuu utakaochezwa siku ya Jumatano ya Sept 19 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba