Japokuwa timu yake imepoteza mchezo wa Ngao ya Jamii, kocha wa Azam FC amesema timu hiyo ipo kamili kwa ajili ya mechi za ligi kuu msimu wa 2012/2013 utakaoanza Sept 15 mwaka huu.

 

Kauli hiyo aliitoa muda mchache baada ya kumalizika kwa mchezo huo ambao Azam FC ilifungwa 3-2 na Simba SC, mchezo uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Kocha Boca alisema timu yake imecheza vizuri katika vipindi vyote lakini wapinzani wao walitumia nafasi walizopata baada ya kusaidiwa na mwamuzi wa mchezo kupata ushindi huo.

 

“Tupo tayari kwa ajili ya ligi kuu, mechi hii imeshakwisha, nawaamini sana wachezaji wangu watafanya vizuri kwenye mechi za ligi na tunaweza kutwaa ubingwa huo” alisema Boca.

 

Aliongeza kuwa kupoteza mchezo huo ni masikitiko kwake lakini amejifunza kitu kwa kuwa hii ni mara yake ya kwanza kuwa na timu katika mechi kubwa ameahidi kurekebisha makosa madogo yaliyojitokeza katika mechi hiyo.

 

Kikosi cha Azam FC kesho kitaelekea mkoani Kagera tayari kwa kuanza mchezo wao wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani humo.

 

Katika mchezo huo Azam FC wakicheza kwa mara ya kwanza Ngao ya Jamii na kuingia katika historia ya mechi hiyo, walikuwa wa kwanza kupata goli lililofungwa na mshambuliaji John Bocco aliyemalizia mpira wa mwisho uliopigwa na Abdulhalim Humud ambaye aliunga mpira wa kona iliyopigwa na Abdi Kassim katika dakika ya pili ya mchezo.

 

Kipre Tchetche aliipatia Azam FC bao la pili katika dakika ya 35 akucheza vema krosi ya mwisho iliyopigwa na Bocco, mabadiliko Azam FC walitoka Tchetche Kipre, Abdi Kassim na Ibrahim Mwaipopo nafasi zao zikachukuliwa na Zahor Pazi, Bolou Kipre na Salum Abubakari ‘Sure Boy’.

 

Mabao ya Simba yalifungwa na Daniel Akuffor dk 45 kwa mkwaju wa penati baada ya mabeki wa Azam FC kunawa mpira eneo la hatari, lakini aliyeanza kuunawa mpira huo alikuwa ni mshambuliaji wa Simba Emanuel Okwii.

 

Dk 68 Emmanuel Okwi alisawazisha bao hilo lakini alikuwa Offside dhahiri na mwamuzi kumuachia lakini pia alipofika kwenye eneo la hatari la Azam FC alitumia mkono kuuweka mpira sawa kabla ya kufunga.

 

 Mwinyi Kazimoto aliandika bao la ushindi kwa Simba baada ya kupiga shuti la mbali na kumaliza mchezo timu hiyo ikipata ushindi wa 3-2.

 

Azam FC Deogratius Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris, Said Morad, Abdulhalim Humud, Ibrahim Mwaipopo/Salum Abubakari 60’, Himid Mao, John Bocco, Tchetche Kipre/Zahor Pazi, Abdi Kassim/Bolou Kipre 68’.

 

Simba, Juma Kaseja, Nassor Masoud, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Pascal Ochieng, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Ramadhan Chombo, Haruna Moshi, Daniel Akuffor na Emmanuel Okwi.