Azam FC inaingia katika historia ya Ngao ya Jamii, kesho kucheza na Simba Uwanja wa Taifa

Masaa machache kabla ya kuchezwa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii, Azam FC wanachukulia mechi hiyo kama sehemu ya mafanikio ya klabu na kuahidi kutoa upinzani mkali katika mchezo huo watakocheza dhidi ya Simba SC.

Azam FC na Simba SC watacheza mchezo wa Ngao ya Jamii siku ya Jumanne, Sept 11, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000.

Timu hiyo inatarajia  kuweka historia mpya kwa kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.

Katibu Mkuu wa Azam FC, Alhaj Nassor Idrissa ameiambia www.azamfc.co.tz kuwa kucheza mchezo huo ni changamoto ya mafanikio kwa klabu na inaonyesha taswira nzuri katika kipindi kifupi tangu ianze kucheza ligi kuu.

Akizungumzia mchezo huo, Alhaj Idrissa alisema mashabiki wategemee mchezo mzuri kutoka kwa Azam FC na kusema mchezo utakuwa mgumu na wenye kuvuta hisia za wengi.

“Ni mchezo utakaovuta hisia tofauti, kwanza tunacheza na bingwa wa ligi, pili ni mechi ya kufungua pazia la ligi kuu na pia ni mara yetu ya kwanza kucheza Ngao ya Jamii” alisema Alhaj Idrissa.

Azam FC inacheza mchezo huo ikiwa ni msimu wake wa nne tangu iingie ligi kuu mwaka 2008, kocha wake, Boris Bunjak ‘Boca’ alisema wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo huo na ligi kuu, hivyo watafanya vizuri

Naye  nahodha wa Azam FC, Ibrahim Shikanda amesema mechi ya Ngao ya Jamii ni heshima kwa klabu hiyo na kuwataka wapinzani wao Simba wetegemee upinzani mkali kutoka kwao.

Mchezo huo utazikutanisha Azam FC iliyokuwa mshindi wa pili itacheza dhidi ya Simba SC ambao walikuwa mabingwa wa ligi kuu msimu uliopita kama ilivyo kanuni ya mechi hiyo huzikutanisha mshindi wa kwanza na wa pili wa ligi kuu.

Shikanda amesema licha ya mchezo huo kuwa mgumu lakini wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha wanatoa upinzani na kutwaa ngao hiyo.

“Ni mara ya kwanza tunacheza Ngao ya Jamii, hii ni heshima kwa klabu na hatua mojawapo tutahakikisha hatupotezi nafasi hiyo kwa kupigana dakika zote za mchezo ili kupata matokeo mazuri” alisema Shikanda.

Mchezaji huyo aliyecheza misimu yote minne amesema dakika 90 ndio mwamuzi wa mchezo huo kwa kuwa wamejipanga vizuri na wachezaji wote wako tayari kwa ajili ya mchezo huo.

Mechi hiyo ni ishara ya ufunguzi wa msimu mpya wa ligi kuu wa 2012/2013 unaotarajiwa kuanza kutimua vumba Jumamosi ya Septemba 15 mwaka huu katika viwanja saba toufauti.

Azam FC inakuwa timu ya nne katika timu za ligi kuu ya Tanzania kucheza kombe hilo ambalo mwanzo lilijulikana kama Ngao ya Hisani, vilabu vilivyocheza mechi hizo ni Simba, Yanga na Mtibwa Sugar.

Kwa mujibu wa  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF asilimia tano ya mapato yatakayopatikana kwenye mechi hiyo (Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya Simba na Azam yatachangia huduma za afya kwenye Hospitali ya Temeke  iliyoko mkoa wa Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ilitolewa na afisa habari wa TFF, Boniface Wambura aliyesema kabla ya kukabidhi, shirikisho litakutana na uongozi wa Hospitali ya Temeke kupanga maeneo ambayo fedha hizo zitatumika kwenye hospitali hiyo.

 Azam FC na Simba SC zinakutana kwa mara ya saba ndani ya mwaka huu wa 2012, timu hizo zilikutana kwenye Kombe la Mapinduzi, mzunguko wa pili Ligi kuu msimu wa 2011/2012, zikakutana mara mbili kwenye mashindano ya Kombe la Urafiki Tanzania, Kombe la Kagame na katika michezo ya BancABC Super 8.