Nahodha wa kikosi cha Azam FC Agrey Moris amewatoa hofu mashabiki na kuwakikishia ushindi katika mchezo wao robo fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya Simba SC.

Azam FC kesho itashuka kwenye Uwanja wa Taifa kusaka nafasi ya kucheza nusu fainali ya kombe hilo,ambapo mshinda itakutana na mshindi wa mchezo kati ya Atletico ya Burundi na AS Vita Club ya Congo DRC.

Agrey alisema wachezaji wenzake wapo katika hali nzuri ya kukabiliana na mchezo huo kwa kuwa wanawajua Simba na watatumia nafasi hiyo kukabiliana nao.

“Itakuwa mechi ngumu lakini tunaamini tutafanya vizuri, Simba tumecheza nao mara nyingi naweza sema tumeshawazoea na kuwajua vizuri,” alisema Agrey.

Wakiwa mazoezini  Azam FC walifanya mazoezi ya kucheza muda mrefu na baadaye kila mcheza alifanya zoezi la kupiga penati huku makipa Deogratius Munishi na Mwadini Ally wakichukua zoezi la kupangua penati hizo.

Wachezaji 17 walipata penati walizopiga huku 7 wakikosa kwa kupiga nje na wengine zikiokolewa na makipa.

Naye kocha msaidizi wa kikosi hicho Kali Ongala alisema wachezaji wote wapo vizuri watakachoangalia atakayeamka vizuri atapagwa kwa ajili ya mchezo huo.

Alisema Abdi Kassim na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ wamerejea katika hali zao za kawaida baada ya kusumbuliwa na maumivu ya mguu.

Kali aliongeza kuwa watatumia vizuri nafasi wanazopata ili kuvuka kuingia nusu fainali ya mashindano hayo.

Katika mchezo wa robo fainali hakutakuwa na muda wa nyongeza kulingana na taratibu za mashindano, baada ya kumaliza dk 90 timu zitapiga penati moja kwa moja.

Kesho itakuwa mara ya tatu Simba na Azam FC zikikutana ndani ya mwezi mmoja, wiki mbili zilizopita walikutana kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Urafiki Tanzania na kutoka sare ya 1-1, na katika mchezo wa fainali hizo walimaliza dk 90 wakitoka sare ya 2-2 lakini Simba walishinda kwa penati ya 3-1.