Timu ya Azam FC imeingia robo fainali ya mashindano ya Kombe la Kagame itakutana na Simba katika mchezo wa  robo fainali ya pili itakayochezwa siku ya Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Pichani juu, Kocha Stewart Hall akitoa maelekezo kwa kiungo wake Rama Chombo, Redondo baada ya kuisha kipindi cha kwanza (picha kwa hisani ya Blogu ya Bin Zubeiry)

Azam FC imeingia hatua hiyo baada ya kuwaondoa kwenye mashindano hayo mabingwa wa zamani wa kombe hilo timu ya Tusker kutoka Kenya ambayo walitoka suluhu kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi uliochezwa leo jioni.

Tusker imeaga mashindano hayo kwa kuwa na pointi mbili sawa na Azam FC na Mafunzo lakini zikatofautiana katika idadi ya magoli, Azam FC na Mafunzo zilipata magoli kwenye mchezo wa kwanza ambao walitoka sare ya 1-1, Tusker wao hawakupata goli kwa kuwa michezo yote miwili walitoka suluhu.

Azam FC inacheza kwa mara ya kwanza mashindano hayo na kuweka historia ya kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ya kimataifa yanayokutanisha mataifa mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, itacheza na Simba huku timu ya Mafunzo itacheza dhidi ya Yanga.

Katika mchezo dhidi ya Tusker, Azam FC walicheza kwa kasi wakiwa na nia ya kupata ushindi ili kuingia robo fainali, katika vipindi vyote walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuweza kupata goli.

Wachezaji John Bocco, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Ibrahim Mwaipopo walionyesha uwezo wao na kuipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya timu ya Tusker.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko dk 77 Mrisho Ngassa aliingia kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche alitoka, dk 87 Khamis Mcha aliyeongoza mashambulizi upande wa Azam FC alitoka nafasi yake ikachukuliwa na Jabir Aziz na dk 90 Gaudence Mwaikimba aliingia kuchukua nafasi ya Bocco.

Tusker walitoka David Makumbi na Joseph Mbugi wakaingia Obadia Ndege na Maurice Odipo, walifanya mabadiliko katika dk 54 aliingia golikipa Samuel Odhiambo kuchukua nafasi ya mchezaji Adrew Mulunga baada ya golikipa Boniface Oluoch kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Issa Kigabo kutoka Rwanda kwa kosa la kushika mpira nje ya eneo lake na kumtendea madhambi John Bocco aliyekuwa kwenye nafasi ya mwisho akitaka kufunga.

Mchezo ukamalizika kwa kutoka suluhu, katika kundi B ambalo Azam FC walikuwa pamoja na Mafunzo, timu hizo zilifungana magoli ya kufunga na kufungwa hivyo kanuni ya waandaaji CECAFA inasema endapo timu zitakuwa sawa kwa kila kitu wataangalia wakati timu hizo zilipokutana timu ya kwanza kufunga ndio itakuwa juu ya nyingine, hivyo Azam FC ikawa ya kwanza na Mafunzo wakawa wa pili.

Azam FC itakutana na Simba ikiwa ni mara ya tano kwa mwaka huu kukutana katika mashindano mbalimbali, Jan walikutana kwenye Mapinduzi Cup, March wakakutana kwenye ligi kuu na wiki mbili zilizopita walikutana mara mbili kwenye mashindano ya Kombe ya Urafiki Tanzania.

Azam FC, Deogratius Munishi, Ibrahim Shikanda, Agrey Moris, Erasto Nyoni, Joseph Owino, Kipre Bolou, Kipre Tchetche/ Mrisho Ngasa (dk 77), Ibrahim Mwaipopo, John Bocco/Gaudence Mwaikimba (90), Ramadhan Chombo na Khamis Mcha/Jabir Aziz (87).

Tusker Boniface Oluoch, Joseph Shikokoti, Jockins Atudo, Humpery Okoti, David Ochied, Joseph Mbugi, David Makumbi, Jerry Santo, Andrew Murunga, Peter Opiyo na Joshua Oyoo.