Wakati mashindano ya Urafiki Tanzania yakielekea pazuri timu ya Azam FC iliyokuwa pungufu jana usiku imelazimishwa sare nyingine ya 1-1 na Simba SC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kwa matokeo hayo Azam FC imefikisha pointi 2 ikiwa nyuma ya Simba na Zanzibar U-23 zenye pointi 4 kila moja, baada ya Zanzibar U-23 kuifunga Mafunzo 1-0, Azam FC inatakiwa kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mafunzo utakaochezwa siku ya Ijumaa uwanjani hapo.

Katika mchezo wa jana Azam FC ilionekana kuuzoea uwanja huo na kucheza kandanda safi muda wote wa mchezo na kuwapoteza kabisa Simba katika mchezo huo uliokusanya mashabiki wengi kutoka visiwani hapa Zanzibar.

Kipindi cha kwanza kilikuwa na kasi muda wote timu zote zikishambuliana huku mshambuliaji mpya wa Azam FC aliyesajiliwa msimu huu George Odhiambo ‘Blackberry’ akionyesha cheche zake na kuwasumbua vilivyo mabeki wa Simba.

Katika  mchezo huo beki aliyekuwa majeruhi ya muda mrefu Joseph Owino ameanza kurejea vyema kwenye kiwango chake baada ya kuwazuia kwa ustadi mkubwa washambuliaji wa Simba waliokuwa wakiongozwa na Kanu Mbiyavanga.

Sehemu ya kiungo Azam FC ilicheza vizuri kwa kuonana huku kiungo mahiri Ramadhan Chombo ‘Redondo’ aking’aa muda wote wa mchezo kwa kuwapoteza vilivyo viungo wa wapinzani wao Simba.

Lakini kiungi mwingine Kipre Bolou alikuwa kwenye kiwango cha juu mno na alicheza kwa ustadi mkubwa sana.

Sifa za pekee ziende kwa Abdulhalim Humud ambaye licha ya kupewa kadi nyekundu baadaye kutokana na kupewa kadi mbili za njano lakini kiwango chake, umahiri wa kukaba na kuwadhibiti washambuliaji wa Simba ulikuwa wa hali ya juu sana.

 Simba walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 35 baada ya beki wa Azam FC, Said Morad kumfanyia madhambi Mbiyavanga wa Simba, faulo hiyo ilipigwa na Musa Mude ikagonga beki ya Azam FC na kurudi uwanjani kabla ya Danny Mrwanda kupachika bao hilo.

Goli hilo halikudumu muda mrefu, katika dakika za nyongeza kipindi cha kwanza mshambuliaji Tchetche Kipre alitengeneza mazingira mazuri kwa kuwatoka mabeki wa Simba na kumpatia pasi ya mwisho Odhiambo aliyesawazisha goli hilo lililompita kipa namba moja wa Simba Juma Kaseja.

Matokeo hayo ya 1-1 yalidumu hadi kumalizika kwa mchezo mchezo huo, katika dakika ya 52 kiungo wa Azam FC mwenye uwezo mkubwa wa kukaba, Abdulhalim Humud alitolewa kwa kadi nyekundu baada kuonyeshwa kadi mbili za njano zilizotokana na kucheza vibaya, tangu muda huo Azam FC walicheza pungufu, maamuzi hayo yalitolewa na mwamuzi wa mchezo huo Ramadhan Isihaka ‘Kibo’.

Mbali na kuwa pungufu Azam FC walijipanga na kukaa vizuri na kuziba pengo la Humud kwa kucheza vizuri wakiendelea kusumbua ngome ya Simba mara kwa mara.

Katika mchezo huo Azam FC walifanya mabadiliko katika dk ya 65 Khamis Mcha Viali aliingia kuchukua nafasi ya Odhiambo mabadiliko hayo yaliimarisha kikosi hicho na kuongeza kasi ya mchezo.

Simba walifanya mabadiliko walitoka Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Musa Mudee, Mbiyavanga na Mrwanda nafasi zao zikachukuliwa na Edward Christopher, Jonas Mkude, Salum Kinje, Abdala Seseme na Uhuru Seleman lakini mabadiliko haya hayakuweza kubadilisha matokeo ya sare ya 1-1.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha msaidizi wa Azam FC, Kalli Ongala aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza katika kiwango kinachostahili na kuwataka waongeze juhudi ili waingie hatua ya nusu fainali.

Azam FC, Mwadini Ally, Samir Haji Nuhu, Said Morad, Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Kipre Tchetche, Michael Kipre, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Gaudence Mwaikimba na George Odhiambo ‘Blackberry’/Khamis Mcha.

Simba Juma Kaseja, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Lino Masombo, Shomari Kapombe, Amri Kiemba/ Edward Christopher, Mwinyi Kazimoto/ Jonas Mkude, Musa Mudee/ Salum Kinje, Mbiyavanga /Abdala Seseme na Mrwanda/ Uhuru Seleman.

Katika kundi A la michuano hiyo timu ya Yanga kutoka Dar es Salaam imeondolewa kwenye mashindano hayo baada ya kukiuka taratibu za mashindano na kuleta kikosi chao cha pili badala ya kulete kikosi cha kwanza, hivyo kundi hilo litabaki na timu za Jamhuri, Super Falcon na Zanzibar All Stars, kabla ya kutolewa Yanga walifungwa 3-2 na Jamhuri.