Baada ya maandalizi ya muda mrefu kikosi cha Azam Academy kesho kitaelekea nchini Burundi kushiriki mashindano ya Rolling Stone yatakayoanza Julai 7 hadi 21 nchini humu.

Azam Academy itaondoka ikiwa kamili kwa kutwaa ubingwa huo ambao mwaka jana walicheza hadi hatua ya fainali na kuwaona JKT Ruvu Shooting wakitwaa baada ya kushinda kwenye muda wa nyongeza kufuatia kwenda sare ya bila kufungana katika muda wa dakika 90.

Akizungumza hivi karibuni Kocha mkuu wa kikosi hicho Nagul Vivek alisema wamejiandaa vya kutosha kwa ajili ya mashindano hayo hivyo kutwaa ubingwa huo ni sehemu ya matarajio yao.

Vivek alisema kikosi kinachokwenda Burundi ni kikosi imara chenye kila hari ya kufanya vizuri kutokana na kupatiwa maandalizi ya kutosha kutoka katika kituo cha mafunzo kilichopo Chamazi Complex.

Alisema wakati wa matayarisho wachezaji walijifunza mbinu mbalimbali za kimpira ikifuatiwa na mazoezi ya uwanjani na gym kwa ajili ya kuwaimara zaidi.

Azam Academy inashiriki kombe hilo ikiwa kwenye D pamoja ya timu ya Mjini Zanzibar, East Kenya, Kiyovu ya Rwanda na waandaaji Burundi.

Msafara wa timu hiyo unaundwa na wachezaji 20 na viongozi watano wa benchi la ufundi, wachezaji walioko kwenye msafara huo ni  Aishi Salum, Dizan Issa, Reina Mgungula, Ismail Adam Gambo, Mohamed Hussein na Kelvin Friday

Wengine ni Ally Kaijage, Braison Raphael, Joseph Kimwaga, Jamir Mchaulu, Farid Musa, Abdul Mgaya, Deogratias James, Ally Aziz, Assad Ally na Ahmed Abbas, Erick Haule, Ahmed Machupa,Ramadhan Swaleh na Mudathir Yahya, viongozi watakaoambatana na timu ni kocha Vivek, kocha msaidizi Iddi Cheche , John, Dr Twalib na Jemedari Said.