Timu ya Azam FC imeanza imelazimishwa sare ya 1-1 na Zanzibar U23 ‘Karume Boys’ katika mchezo wa kwanza wa kombe la Urafiki Tanzania, uliochezwa kwenye uwanja wa Amaan Zanzibar.

Azam FC inashiriki mashindano hayo ikiwa kundi B pamoja na timu za Zanzibar U23, Mafunzo na Simba ya SC, kundi A linaundwa na Yanga, Super Falcon, Zanzibar Stars na Jamhuri.

Katika mchezo huo Azam FC ilianza na kikosi cha wachezaji wasiopata nafasi kikosi cha kwanza, wachezaji hao walicheza vizuri na kuonyesha uwezo wao.

Wachezaji hao walioanza pamoja na wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu golikipa Deogratius Munishi na mshambuliaji George Odhiambo ‘Blackberry’ ulisaidia timu hiyo kucheza vizuri muda wote wa mchezo. Deo Munishi alionesha kuwa ni lulu ndani ya kikosi cha Azam FC.

Kikosi hicho mwanzo wa mchezo kilipata wakati mgumu kutokana na uwanja huo kutokuwa mzuri lakini muda ulivyoendelea wachezaji walizoea na kucheza vizuri.

Karume Boys walipata goli katika dakika 45 kupitia kwa mkwaju wa penati iliyopigwa na Ibrahim Hamis baada ya beki wa Azam FC kumtendea mdhambi Mwinyi Amer.

Kipindi cha pili Azam FC walifanya mabadili walitoka Abdulghan Gulam, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Odhiambo na Zahor Pazi nafasi zao zikachukuliwa na Abdulhalim Humud, Ramadhan Chombo, Michael Kipre, Kipre Tchetche na Gaudence Mwaikimba.

Mabadiliko hayo yaliimarisha na kuongeza kasi ya mchezo hali iliyopelekea mabeki wa U23 washindwe la kufanya na kuiacha Azam FC ikisawazisha bao hilo katika ya 68 kupitia kwa Kipre Tcheche aliyemalizia kazi nzuri ya Ramadhan Chombo.

Kwa matokeo hayo Azam FC pamoja na Karume Boys zimegawana pointi moja moja, Simba ikiongoza kundi hilo kwa kuwa na piointi tatu baada ya kuifunga Mafunzo 2-1.

Kesho Jumatano, Azam FC watashuka tena kwenye uwanja huo kucheza dhidi ya Simba huku Mafunzo watavaana na vijana wa Karume Boys.

Azam FC, Munishi, Samir Haji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Joseph Owino, Luckson Kakolaki, Gulam/Humud, Jabir/Chombo, Mwaipopo/Michael, Odhiambo/Kipre, Pazi/ Mwaikimba na Khamis Mcha.

Karume Boy, Khalid Mahadhi, Salum Said, Seleman Haji, Ramadhan Abdalah, Idrisa Abdulrahim, Haji Mwinyi, Makame Hamad, Ibrahim Hamis, Nasor Maftah, Mwinyi Amer na Seif Abdalah.