Japokuwa wamefungwa 2-1 lakini timu ya Azam Academy wamewapelekesha vilivyo kaka zao Azam FC kwenye mchezo wa kujipima nguvu uliopigwa jana asubuhi, kwenye uwanja wa Azam, Chamazi.

Timu hizo zinajiandaa na mashindano, Academy wanajiandaa na mashindano ya Rollingstone 2012 yatakayofanyika nchini Burundi wakati Azam FC wao wanajiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame yatakayofanyika Dar es Salaam mwezi ujao.

Academy walicheza kandanda safi muda wote wa mchezo na kuwapa wakati mgumu Azam FC kutokana na uwezo wa wachezaji hao.

Vijana hao walio chini ya miaka 20 ingawa wengi wao ni chini ya miaka 17 wamecheza mchezo  huo siku moja baada ya kuifunga timu ya Iringa United kutoka mkoani Iringa mabao 7-0.

Katika mchezo dhidi ya Azam FC ambao Academy walifungwa 2-1, Academy walikuwa  wa kwanza kupata bao la mapema katika dakika ya tano ya mchezo kupitia kwa Joseph Kamwaga aliyeachia shuti lililomshinda kipa Deogratias Munishi ‘Dida’ wa Azam FC. Kimwaga ambaye anaaminika kuwa ndiye winga mwenye kasi zaidi nchini kwa sasa ambeye pia anachezea timu ya taifa ya Under 20 alikuwa mwiba kwa mabeki wa Azam FC muda wote wa mchezo.

Goli hilo lilidumu hadi mapumziko huku timu hiyo ikiwanyanyasa kaka zao kwa kuwaonyesha uwezo wao imara uliojengeka kutokana na mazoezi bora wanayopata chini ya makocha wao Nagul Vivek na Iddi Cheche.

Azam FC walitafuta nafasi ya kushinda lakini timu hiyo iliyocheza kipindi cha kwanza ikiongozwa na Gaudence Mwaikimba haikuweza kubadilisha matokeo hayo.

Kipindi cha pili kilianza vizuri vijana walikuja kwa kasi na kuzuia mashambulizi ya kaka zao Azam FC, lakini dakika mbili za mwisho makosa ya benchi la ufundi la Academy ya kubadilisha timu yao ili kutoa nafasi kwa wachezaji zaidi kupata nafasi ya kucheza yalipelekea Azam FC kutumia nafasi hiyo kusawazisha goli na kuongeza goli la Ushindi.

Goli la kwanza kwa Azam FC liliwekwa wavuni na mshambuliaji George ‘Blackberry’ Odhiambo kwa shuti la pembeni na goli la ushindi lilifungwa na mshambuliaji Zahoro Pazi kwa shuti la mbali nje ya eneo la penati.

Timu hizi zitarudiana siku ya Jumamosi Asubuhi ambapo kambi zote mbili zimetamba kushinda mchezo huo.

Kabla ya hapo hapo kesho asubuhi Azam Academy itashuka kwenye uwanja wa JKT Ruvu kukwaana na JKT Ruvu.