CHAMA cha mpira wa miguu Zanzibar (ZFA) kitaandaa mashindano ya mpira ya soka ya Kombe la Urafiki ambayo yatazikutanisha timu za Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia Julai 1 mpaka Julai 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Aman.

Taarifa hizo za mashindano hayo zilitolewa jana kwenye Hoteli ya Ocean View wakati Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Zanzibar,   Said Ali Mbarouk alipokuwa akizindua Kamati maalumu kwa ajili ya kusimamia mashindano hayo yatakayokuwa na sura ya mungano.

Kamati hiyo ina wajumbe saba na itaongozwa na Mwenyekiti wake Ibrahim Raza na Katibu ni Suleiman Muhamoud Jabir.

Jumla ya timu nane kutoka Zanzibar na tatu Tanzania bara, ambapo kwa upande wa Zanzibar ni Jamhuri, Mafunzo, Miembeni Fc, Super Falcon na timu ya Taifa iliyo chini ya umri wa miaka 20 na kwa upande wa Bara ni Simba, Yanga na Azam FC.

Mshindi wa kwanza wa mashindano hayo atakabidhiwa kikombe pamoja na sh 10 milioni, mshindi wa pili atapata sh 5 milioni na mshindi wa tatu atapata sh 3 milioni.

Mashindano hayo yamedhaminiwa na Hoteli ya Ocean View Hotel na Royal Furniture kwa jumla ya sh 160 milioni.

Mbarouk alisema mashindano hayo yatatoa fursa ya kuzijengea uwezo timu zote za Tanzania ambazo zina nafasi za uwakilishi wa kikanda barani Afrika na Mashindano ya Chalenji.

Waziri huyo aliitaka Kamati hiyo kuyafanya mashindano hayo kuwa ya kuvutia na kuwashawishi Wadau kudhamini Soka la Zanzibar.

“Kama mashindano haya tukiyatumia vizuri basi nakuhakikishieni tutapata wadhamini wengi wa ligi zetu mbali mbali,” alisema Mbarouk.

Naye Makamu wa Rais wa Chama cha soka Zanzibar (ZFA), Ali Muhammed alisema mashindano hayo yataendeleza udugu uliopo kati ya watu wa Tanzania Bara na Visiwani na kudumisha ushirikiano.

Muhammed alisema atahakikisha mashindano hayo yanakwenda vizuri kwa lengo la kuwafanya wadhamini wayaamini na kujitokeza kwa wingi katika kudhamini mashindano mengine.

“Lazima fursa hii tuitumie vizuri katika kulinda imani  za wadhamini wa soka letu,” alisema Muhammed.

Source Gazeti la Mwananchi