Kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall anatarajiwa kuwasili nchini siku ya Jumatatu asubuhi kwa ajili ya kuanza program ya maandalizi kwa mashindano ya kombe la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Stewart alikuwa nchini Uingereza kwa mapumziko baada ya kumaliza msimu uliopita kwa mafanikio ya kutwaa medali ya fedha kwa kuwa  washindi wa pili wa VPL.

Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa jana ameiambia tovuti ya www.azamfc.co.tz  kuwa  wataanza mazoezi jioni kutokana na kocha huyo kurudi asubuhi ya siku hiyo.

Akizungumzia wachezaji wengine alisema, wachezaji wote wa kimataifa wameshawasili tayari kwa kuanza mazoezi hayo wakiwa pamoja na wachezaji wengine. Mazoezi hayo yatafanyika  kwenye uwanja wa Azam Chamazi jijini Dar es Salaam.

Idrissa aliongeza kuwa wachezaji waliopo timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ watajiunga mara baada ya kumaliza michezo yao, na wale wa Zanzibar Heroes watarejea nchini baada ya kumaliza michezo ya Kombe la Dunia kwa nchini ambazo sio wanachama wa FIFA.

Aliwataja wachezaji waliowasili kuwa ni George Odhiambo na Ibrahim Shikanda kutoka nchini Kenya ambao wote waliingia Alhamis, Tchetche Kipre na Michael Kipre kutoka nchini Ivory na Joseph Owino wa Uganda.

Idrissa alisema wachezaji wa Tanzania nao wameshaandaa mazingira kwa ajili ya kuanza mazoezi hayo wakiwemo vijana kutoka Azam Academy ambao wamepanda kuicheza timu kubwa, Aishi Salum, Juckson Wandwi, Dizana Issa, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ na Joseph Kimwaga.

Aidha Idrissa alisema Azam Academy wameshaanza mazoezi siku ya Ijumaa isipokuwa wacheza watatu ambao bado hawajawasili kujiunga na timu hiyo.