Taarifa zaidi Kwa mujibu wa Blog ya BIN ZUBEIRY ( http://bongostaz.blogspot.com/2012/05/mafisango-kuagwa-asubuhi-kesho-leaders.html ), MWILI wa kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango wa Simba, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya gari maeneo ya Tazara, Dar es Salaam unatarajiwa kuagwa kesho saa 2 asubuhi katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam.

Meneja wa Simba SC, Nicodemus Menard Nyagawa ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, baada ya zoezi la kuagwa kukamilika, mwili huo utasafirishwa kwa ndege ya shirika la ndege ya kenya, KQ kwenda Kigali, Rwanda kwa shughuli za mazishi.


Nyagawa ametoaq wito kwa wapenzi wote wa Simba kujitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa marehemu Mafisango, aliyekuwa kiungo tegemeo wa klabu hiyo katika msimu wake mmoja tu wa kuichezea tangu ajiunge nayo, akitokea Azam FC.   


Mafisango alifariki kwa ajali ya gari akiwa anarejea nyumbani kwake, kutoka disko na kwa sasa mwili wake upo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.


Nyagawa alisema Mafisango aliyekuwa anaendesha mwenyewe gari lake, alikuwa anajaribu kumkwepa dereva wa pikipiki na kwa  bahati mbaya akaingia mtaroni na kuumia kabla ya kufariki dunia


Mafisango aliyekuja nchini mwaka juzi na kujiunga na Azam kabla ya kuhamia Simba mwaka jana, alizaliwa Machi 7, mwaka 1987 mjini Kinshasa, DRC alikoanzia soka kabla ya kuhamia Rwanda, ambako baadaye alichukua uraia wa nchi hiyo.


Kabla ya kuja Tanzania alichezea APR ya Rwanda. Mechi ya mwisho Mafisango kuichezea Simba ilikuwa dhidi ya Al Ahly Shandy nchini Sudan Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penalti 9-8, kufuatia sare ya jumla ya 3-3.


Hadi anafariki dunia, Mafisango alikuwa ni tegemeo Simba katika safu ya kiungo na jana tu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nange 'Kaburu' alisema kiungo huyo yupo kwenye mpango wa kocha wa kikosi cha msimu ujao
Pamoja na kucheza kama kiungo, Mafisango pia anamudu kucheza nafasi ya beki wa kushoto na beki wa kati.


Japokuwa alikuwa kiungo, lakini pia alikuwa hodari wa kufunga mabao na msimu huu imeshuhudiwa akiifungia Simba mabao 11 katika Ligi Kuu na manne kwenye Kombe la Shirikisho.


Wakati Simba ikijiandaa kwenda kurudiana na ES Setif katika mechi ya hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho, ilitaka kumuacha kiungo huyo baada ya kumsimamisha kwa utovu wa nidhamuingawa baadaye busara ilitumika akasafiri na timu baada ya kuomba radhi.


Tuhuma aza utovu wa nidhamu kwa Mafisango zilianza kumuandama tangu akiwa Azam FC na ndiyo sababu kubwa ya klabu hiyo kumuacha aende Simba licha ya kwamba ilimsajili kwa gharama kubwa kutoka APR ya Rwanda.


Pamoja na yote, ndani ya Uwanja Mafisango alikuwa suala jingineanajituma mno na alikuwa ana msaada mkubwa timu. Kwa sababu ya nidhamu aliachwa hadi timu ya taifa, Amavubilakini kwa soka yake maridadi akiwa Simba, kocha mpya wa timu hiyo Milutin Sredojevic 'Micho' safari hii alimuita kikosini, ingawa kabla ya kupanda ndege kurejea nyumbani kuitikia wito huo, umauti umemkuta


Poleni wana Simba wote, pole kwa ndugu, jamaa na familia ya Mafisango. Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe milele. Amin. Mungu aiweke pema peponi Roho ya Marehemu