Mwenyekiti wa Azam FC Abubakara Bakhresa amewapongeza wachezaji na viongozi wa Azam FC kwa kukamilisha dhamira hiyo pamoja na kuridhishwa na mafanikio ya klabu yake.

“nimefurahi na kuridhishwa na mafanikio ya klabu, ndani ya misimu minne, msimu wa kwanza tulikuwa tunajilinda tusishuke daraja lakini kwa kipindi hiki tumeweza kuwa katika nafasi ya pili ni mafanikio makubwa kwetu” alisema Bakhresa.

Mwenyekiti alijivunia juhudi na nidhamu imechangia kuifikisha timu katika mafanikio hayo kwa kuwa wachezaji wameonyesha nidhamu kubwa na wale walioenda kinyume walichukuliwa hatua.

Akizungumzia changamoto waliyokutana nayo msimu huu Bakhresa alisema klabu ilisimama kidete kupambana na kila hila iliyokuwa inatengenezwa makusudi kuharibu jina la Azam FC kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuharibu mechi ili kuishushia heshima klabu.

Alisema kuwa na umoja kati ya viongozi na juhudi za wachezaji wameweza kupambana na hali hiyo hadi mwisho ambapo timu imekamilisha lengo lake kwa kufanya vizuri katika mechi zake.

Akielezea muenendo wa soka nchini, alisema kipindi cha sasa soka linakua na kutoa ajira kwa wachezaji alitolea mfano kwa Azam FC wameweza kuwapa mahitaji muhimu ambayo pengine si rahisi kuyapata katika vilabu vya nje ya nchi.

“Azam FC inanufaika na kutoa ajira kwa vijana kupitia michezo na wachezaji wananufaika kwa kuichezea Azam FC” alisisitiza Bakhresa.

Mbali na mafanikio Mwenyekiti alimpongeza mshambuliaji wa klabu hiyo John Bocco kwa kumaliza ligi akiwa mfungaji bora na mchezaji bora wa klabu hiyo na kuvunja rekodi kwa kufikisha magoli 19.

Alisema mafanikio ya Bocco yamechangiwa na timu nzima, bila kuwa na wachezaji wengine asingekuwa katika nafasi hiyo aliwapongeza na kuwashukuru wachezaji kwa kufanikisha mafanikio ya Bocco.

Amefurahishwa na kuutekelezaji wa mapema uliofanywa na klabu hiyo ambao ni kuwa na kituo cha mazoezi 'Training centre' chenye uwanja wa kisasa, gym yenye kiwango cha hali ya juu pamoja na hostel za kisasa ambazo zinatumiwa na timu ya vijana (Azam Academy), na kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi 2012.

Alisema hayo ni sehemu ya mipango ya klabu ya kuleta mapinduzi ya sika nchini na kauhidi kuwa timu itaendalea kwa kufanya vizuri katika ligi ijayo pamoja na mashindano ya kimataifa.

Mwenyekiti ametangaza rasmi dhamira ya msimu ujao ni kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom, kufanya katika michezo ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika na kombe la Afrika Mashariki na Kati 'CECAFA'.

Amewaaga wachezaji kwa kuwatakia mafanikio mema wakat huu wa likizo, watumie vema likizo zao kwa kulinda vipaji hivyo na kuwatakia maisha mema wachezaji watakaoachwa na timu hiyo.

Aliwashukuru wote waliohusika kuifikisha timu katika hatua hiyo na kutambua mchango wa waandishi wa habari za michezo nchini kwa kuwapa vyeti vya shukrani.

Hafla ilihuduriwa na viongozi wa Shirikisho la Mpira nchini TFF, wawakilishi wa vilabu vya ligi kuu, Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azan na vyombo vya habari.

Azam FC iliingia ligi kuu misimu minne iliyopita, msimu wa kwanza 2008/09 ilimaliza ikiwa nafasi ya nane, msimu wa pili 2009/2010 na msimu wa tatu 2010/2011 timu ilimaliza ikiwa katika nafasi ya tatu na msimu huu 2011/2012 imemaliza msimu ikiwa nafasi ya pili.