Leo katika dimba la taifa (National Stadium) kutafanyika mchezo wa marudio kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar SC, Mchezo huu unarudiwa kwa kuwa viongozi wetu wa mpira wameamua kutumia busara zaidi kwenye maamuzi badala ya kufuata kanuni. Kikanuni ilikuwa dhahiri shahiri Mtibwa Sugar angeteremshwa daraja kwa kugomea Penati ambayo ni sehemu ya mchezo huku wakimshambulia mwamuzi hivyo kuvuruga mchezo. Sijua ni mechi ngapi za ligi kuu ya nchi nyingine zimewahi kurudiwa kwa sababu kama hizi zilizoainishwa na viongozi wetu?

Tanzania ni nchi ambayo viongozi wake wanatumia sana busara kuliko kanuni walizozitengeneza wenyewe na busara yao ikawaongoza kulihamisha pambano hili toka Chamazi yalipo makazi ya Azam FC hadi Uwanja wenye matuta wa Ruvu Shooting Mabatini Pwani, Azam FC ikatumia busara kuamua kubeba gharama kubwa za uwanja wa Taifa ili pambano hilo lichezwe kwenye uwanja mzuri na wenye usalama.

Swali ambalo Webmaster anajiuliza ni kuwa, Je kulitokea janga gani la kiusalama Chamazi Stadium hadi mwamuzi kuvunja mchezo hivyo kulazimu mchezo kuhama toka Chamazi? Huu ulikuwa mchezo wa nyumbani wa Azam FC ambayo katika mchezo wa kwanza ilisafiri hadi Manungu. Ni kanuni gani inayosema kuwa mchezo ukivunjika kwa makosa ya mwamuzi utarudiwa na kuhamishwa uwanja na kama ipo ni busara gani iliyotumika kutengeneza kanuni ya namna hiyo? Hili swali webmaster analiacha kama changamoto kwa viongozi wetu ili warekebishe kanuni zao.

Rai ya mwisho toka kwa webmaster kwa viongozi wa TFF ni kupitia kanuni zao, kuziboresha, na kuendesha ligi kwa kufuata kanuni na si kutumia busara ya nani ataathirika kwa kanuni kufuatwa.

Azam FC imeamua kupeleka timu uwanjani siyo kwa sababu haijui sheria na haki zake, siyo kwa kuwa haijui kuwa haki ipo upande wake na kama tukikata rufaa tutashinda ila kwa sababu tunaupenda mchezo wa mpira na tunapenda amani kwenye michezo. Tutacheza mchezo wa leo kwa sababu tunataka kusaidia kumaliza malumbano yasiyo na msingi ambayo watu wanaamua kutumia busara badala ya kufuata kanuni.

Wahenga ni welevu sana wametupa misemo yenye kubeba ujumbe murua sana, leo nitaandika hitimisho kwa kutumia misemo na nahau nikijaribu kukumbuka na kuenzi tunu niliyopewa wa waalimu wangu wa lugha, Wahenga walisema Maji ukiyavulia nguo huna budi uyaogeAzam FC imeshavaa jezi na haina budi kucheza mpira wa ushindani ikiwa na malengo ya kupata mafanikio, vikwazo hivi tunavichukulia kama changamoto

Wahenga wanaendelea kutuambia “Nyimbo ya Kufunzwa haikeshi Ngoma”, Mtibwa Sugar ikishuka dimbani huku ukiwa imevaa koti la timu pinzani  kama ilivyokuwa kwa Toto Africa. Hapana shaka kuwa itapigana kwa nguvu zote ili kuisaidia hiyo timu ipate ubingwa lakini ubora wa Azam FC upo juu na itaishia kuwa kama nyimbo ya kufunzwa.

WaHenga walisema, Ukianza safari watakutia moyo lakini ukionesha mafanikio vitaibuka vikwazo, ligi kuu msimu huu kumeibuka vikwazo vingi dhidi ya Azam FC na maneno ya  kutunga ili mradi tuu kutukatisha tamaa lakini tunasema TUNASONGA MBELE, HATURUDI NYUMA