Mchezo kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar uliochezwa leo Uwanja wa Azam Chamazi, ulivunjika katika dakika ya 88 baada ya wachezaji wa Mtibwa kukataa kuingia uwanjani.

Tukio hilo lililoleta sura tofauti ya mchezo huo lilitokea baada ya Azam kupata penati iliyoamriwa na mwamuzi Rashid Msangi wa Mpwapwa lakini wachezaji wa Mtibwa walionekana kupinga maamuzi hayo hali iliyopelekea kuvunjika kwa mchezo huo.

Kutokana na tukio hilo maamuzi yatatolewa baada ya mwamuzi kufisha repoti ya mchezo huo katika kamati ya mashindano na kujadiliwa na kamati ya Ligi kuu.

Sheria za soka zipo wazi, timu inapogomea mchezo, wapinzani wao wanapewa ushindi wa pointi tatu na magoli matatu. Kwa hali hiyo ni kama Azam FC imeshinda mchezo wa leo.

Mchezo ulianza vizuri Azam walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya kwanza lililofungwa na Mrisho Ngassa aliyeweka mtoka kipa wa Mtibwa Deogratius Munishi Dida na walinzi wake na kuandika bao hilo.

Kipindi cha pili Mtibwa walisawazisha goli hilo katika dakika ya 63 kupitia kwa nahodha Salum Swed aliyepiga mpira wa adhabu uliogonga mabeki wa Azam na kutinga wavuni, hadi kuvunjika kwa mchezo huo timu zote zilikuwa sare ya 1-1.

Katika mchezo huo mchezaji wa Mtibwa, Said Rashid Bahanuzi alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumtendea madhambi kiungo wa Azam FC, Salum Aboubakar 'Sure Boy' katika dakika ya 58.

Mchezo huo ambao kama ungemalizika kwa matokeo hayo, Azam FC walikuwa wanapunguza idadi ya pointi zitakazowawezesha kukaa katika nafasi ya pili itakayowapa fursa ya kucheza mashindano ya kimataifa.

Mechi inayofuata kabla ya kumaliza mzunguko huu Azam FC watacheza na Toto African katika uwanja huo, April 30 mwaka huu na mchezo wa mwisho utakuwa Mei 5 dhidi ya Kagera Sugar.