Azam FC Jumatatu tarehe 23 April 2012 itaingia katika historia mpya endapo itafanikiwa kuifunga Mtiwa Sugar. Historia inayotarajiwa na Azam FC kesho ni kushika nafasi ya pili na hivyo kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Afrika. Endapo Azam FC itashinda kesho basi itafikisha pointi 53, idadi ambayo haiwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote ukiondoa Simba ambayo tayari ina pointi 56.

Kutinga kwenye mashindano ya Afrika kunaondoa mazoea ya zaidi ya miaka 10 iliyopita ambapo vilabu vya Simba na Yanga vilikuwa vimetawala mpira wa Tanzania na kufanya nafasi mbili za juu kama mali yao.

Ni kama siasa za chama kimoja vile, mpira wa Tanzania ulikuwa umeshikwa na vilabu vikongwe vya Simba na Yanga kiasi cha kutengeneza mgando wa mawazo kwa mashabiki wengi nchini kuwa haiwezekani na haitakuja kutokea kwa timu nyingine nje ya wababe hao wa kariakoo kuweza kupata nafasi ya kuwakilisha nchi.

Ikumbukwe kuwa kuna wakati huko nyuma vilabu vya Prisons na Mtibwa Sugar vilishika nafasi za juu lakini historia inaonyesha kuwa kulikuwa na migogoro mikubwa Simba au Yanga iliyotoa nafasi kwa vilabu vya Prisons na Mtibwa na kama hali isingekuwa hivyo leo tungekuwa tunasherekea kuondoa zaidi ya miaka 20 ya utawala wa Simba na Yanga.

Mafanikio ya Azam FC yameanzia kuanzishwa kwake mwaka 2006 na hadi kupanda ligi kuu msimu wa 2008. Mafanikio ya timu hii hayawezi kukamilika bila kuwataja watu kama Boniface Pawasa, Stephen Nyenye, Yahaya Tumbo, Shaabani Kisiga, Said Swedi, Iddi Abubakar, Khamis Japhar nk ambao walifanya kazi kubwa huko nyuma chini ya uongozi wa watu kama Katibu mkuu Nassor Idrissa, Selemani Mabehewa na mwenyekiti Abubakar Bakhresa.

Leo picha ya nje ya Azam FC wanaonekana watu wapya lakini viongozi na wachezaji hawa wapya wamerithi misingi mizuri iliyoachwa na viongozi wa mwanzo kama Habib Kondo, Itamar Amorin, Mohammed King, Sylverster Marsh, Naider Dos Santos, Meneja Jeshi, Abubakar Mapwisa, nk.

Kwenye kikosi cha Azam FC kuna nyota kama Luckson Kakolaki, Salum Abubakar na John Bocco ambao walikuwa sehemu ya kuileta timu ligi kuu na mpaka leo ni wachezaji muhimu ndani ya kikosi. Pongezi za dhati kwao. Duniani kote wachezaji kama hawa huthaminiwa sana na ndivyo klabu ya Azam FC inavyofanya kwao.

Azam FC ambayo ni timu pekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na kituo cha michezo chenye ubora wa hali ya juu cha Chamazi huku uwekezaji wake ukiendelea kufanyika kwa awamu inategemewa na wengi kutikisa kwenye soka la Afrika kama ilivyo kwa TP Mazembe.

Tayari bodi ya wakurugenzi wa Azam FC wameweka wazi kuwa, dhamira ya kuanzishwa kwa Azam FC ni kuondoa dhana kuwa watanzania hatuwezi na stahili yetu ni jina la “kichwa cha mwenda wazimu”. Uongozi wa Azam FC chini ya mwenyekiti wake umedhamiria kugeuza hali hii na kuifanya Tanzania nchi ya kuogopwa na kuheshimika kwenye soka la Afrika. Kufikia malengo hayo inahitaji muda, kuungwa mkono na wadau na uvumilivu kitu ambacho kimeoneshwa kuwa kinawezekana ndani ya Azam FC.

Kuna mtu mmoja ambaye ametoa mchango mkubwa sana kwenye mafanikio ya Azam  FC msimu huu, huyu ni mwalimu Stewart Hall, mwalimu huyu ni mjuzi sana, anafanya kazi zake kwa uweledi wa hali ya juu ndani na nje ya uwanja, Azam FC inajivunia kuwa na mtu kama yeye. Uwepo wake unatengeneza imani kubwa kwa klabu kutawala soka la Afrika katika kipindi kifupi kijacho.

 Kila la Kweli Azam FC hapo Jumatatu katika safari ya historia mpya