Dakika 50 zilitosha kuipatia Azam FC pointi tatu muhimu na kuepeleka nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya Vodacom baada ya kuifunga Ruvu Shooting Stars 1-0 kwenye mchezo uliochezwa leo uwanja wa Azam Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Azam FC imeendeleza mfululizo wa ushindi na kujiimarisha na kuwa katika nafasi ya kutwaa ubingwa au nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 44.

Ushindi huo kwa Azam bado unavuka rekodi tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo hii ni mara yake ya kwanza kufikisha pointi 44 huku wakiwa na michezo mitano iliyosalia kumaliza ligi kuu.

Katika mchezo huo goli pekee lilipatikana katika dakika ya 50 kupitia kwa mchezaj Mrisho Ngasa aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ibrahim Mwaipopo, Ngasa alimalizia kazi nzuri ya John Bocco aliewatoka mabeki wa Ruvu Shooting na kupiga mpra uliotua kwa Ngasa na kumshinda kipa Benjamin Haule wa Shooting aliyekuwa nyota wa mchezo wa leo.

Mchezo ulikuwa wa kasi na ulionekana mgumu kwa pande zote, kipindi cha kwanza kila timu ilifanya mashambulizi lakini hawakupata ushindi, Bocco na Mwaipopo wa Azam walishindwa kutumia nafasi walizopata hivyo timu zikaenda mapumziko zikiwa 0-0.

Kipindi cha pili  Mwaipopo alitoka nafasi yake ikachukuliwa Ngasa aliyebadili mchezo na kupelekea kupatikana kwa goli hilo.

Mabadiliko mengine dk 69 alitoka Abdi Kassim akaingia Abdulhalim Humud na dk 77 Khamis Mcha aliingia kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche.

Kocha wa Azam, Stewart Hall amezungumzia ushindi huo kuwa ni sehemu ya mipango yake kutaka kushinda michezo yote iliyobaki na kusema kiwango cha wachezaji wake katika mchezo hakikuwa cha juu kutokana na Shooting kuonyesha upinzani mkali muda wote wa mchezo.

Alisema mechi zilizopita zilikua rahisi ukilinganisha na mchezo huo, kwa kuwa hawakupata magoli mengi kama ilivyokuwa michezo mitatu iliyopita ambapo walipata magoli kumi katika michezo hiyo ambayo walizifunga Villa Squad 4-1, Coastal Union 3-0 na Yanga 3-1.

Azam, Mwadini, Waziri, Nyoni, Aggrey, Luckson Kakolaki, Michael Kipre, Tchetche/Mcha(dk 77), Mwaipopo/Ngasa(dk 45), Abdi Kasim/Humud (dk 69), Salum Sure Boy na Bocco.