Ikitafuta rekodi mbili za klabu Azam FC leo imejikuta ikipata rekodi nne kwa mpigo baaada ya kuisasambua Yanga 3-1 katika mchezo mkali wa ligi kuu ya Vodacom.

Pichani mshambuliaji John Bocco akishangilia goli lake la 15 msimu huu

Rekodi ya kwanza imewekwa na mshambuliaji John Bocco ambaye leo amefunga magoli mawili na kufikisha jumla ya magoli 15  baada ya kushuka dimbani mara 18. Rekodi yake ni magoli 14 Msimu wa 2009/2010.

Endapo Bocco atafunga magoli mawili tuu kwenye mechi sita zilizosalia basi ataweka rekodi ya Klabu ambayo inashikiliwa na mrisho Ngasa aliyefunga magoli 16 msimu uliopita. Ngasa hivi sasa ana magoli mawili tuu. Rekodi ya juu ya magoli  ligi kuuni inashikiliwa na Boniface Ambani na Mussa Mgosi ambao waliwahi kufunga magoli 18.

Rekodi ya pili kwa Azam FC ni kufikisha pointi 41 kwenye ligi kuu tena ikiwa imecheza mechi 20 tuu. Azam FC ambayo huu ni msimu wake wan ne kwenye ligi kuu haijawahi kufikisha pointi 41 katika historia yake tangia ianzishwe.

Katika msimu wake wa kwanza wa ligi kuu msimu wa 2008/2009. Azam FC ilimaliza na pointi 24, Msimu uliofuata wa 2009/2010 azam FC ilimaliza ligi ikiwa na pointi 34 na msimu uliopita wa 2010/2011 Azam FC ilimaliza ligi na pointi 40. Ukiangalia rekodi utaona kuwa timu imekuwa ikiimarika taratibu na msimu huu kitendo cha kufikisha poiti 41 huku ligi iliwa bado inaendelea kimetoa matumaini makubwa sana.

Rekosi ya tatu ni kuifunga Yanga mara nne mfululizo. Rekodi hii imeanzia kwenye ushindi wa 1-0 kwenye raundi ya kwanza VPL na ikafuatia ushindi wa 2-0 kwenye mechi ya kirafiki ya Hisani kabla ya kuitandika Yanga 3-0 na kuisukumiza nje kwenye mashindano ya Mapinduzi cup.

Yanga walikuja kwenye mechi hii ya leo wakijigamba kuwa wao ndiyo wenye ligi na lazima waifunge Azam FC kwenye mechi ya leo na kuthibitisha kuwa wao sit u mabingwa wa Afrika Mashariki na kati bali pia ni mabingwa Tanzania lakini hali ilikuwa tofauti baada ya kupokea kichapo cha 3-1.

Rekodi ya nne ni kuongoza ligi hata kama Azam FC imecheza michezo miwili zaidi ya Yanga na Simba. Tangia Azam FC ianzishwe, haijawahi kuongoza ligi wakati ligi imeingia raundi ya pili kwa namna yoyote ile. Hii ni rekodi kwa Azam FC na kutokana na kubanana kwenye nafasi ya juu. Ligi ya Tanzania inakuwa na ushindani na mwamko mzuri zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma.

Kiungo Michael Kipre alifungia Azam goli lake la kwanza ligi kuu Vodacom tangu ajiunge na timu hiyo huku mshambuliaji John Bocco akizidi kuongeza idadi ya magoli na kuwaacha mbali wafungaji wengine katika ligi kuu. Kipre alifunga goli la pili huku Bocco akifunga la kwanza na la tatu.

Azam walianza mchezo huo kwa kasi dakika ya 4 Bocco aliiandika goli la kwanza katika mchezo huo kwa shuti lililompita kipa wa Yanga, Shaban Kado.

Baada ya goli hilo mchezo ukabadilika na kuwa wa vurugu baada ya mchezaji wa Yanga, Haruna Niyonzima kutolewa kwa kadi nyekundu kutokana na kuonyeshwa kadi mbili za njano na mwamuzi Israel Nkongo wa Dar es Salaam.

Wachezaji wa Yanga walimzonga na kumpiga mwamuzi huyo hali iliyopelekea mchezaji Nadir Haroub naye kutolewa kwa kadi nyekundu, mpira ukasimama kwa dakika tano na kuendelea katika dakika ya 20.

Kipindi cha pili Azam walianza kwa mabadiliko alitoka Ibrahim Mwaipopo nafasi yake kuchukuliwa na Abdi Kassim aliyebadili mchezo.

Michael Kipre dk 54 akatumia vema mapungufu ya Yanga na kufunga goli la pili kwa shuti la mbali na kumfanya kipa wa Yanga, Kado asijue la kufanya.

Dk 76 Bocco alikamisha kalamu ya magoli kwa kufunga goli la tatu akimalizia krosi kazi ya kipre Tchetche ambaye alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Yanga leo. Hii imemfanya Bocco kuendelea kuongoza idadi ya wafungaji akiwa na magoli 15 hadi hivi sasa.  

Goli pekee la Yanga lilifungwa na Hamis Kiiza baada ya kucheza vizuri na Shadrack Nsajigwa.

Kwa ushindi huo Azam imefikisha pointi 41 na kuongoza ligi ikifuatiwa na Simba yenye pointi 40 huku Yanga akibaki na pointi zake 37.

Azam, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Said Moradi, Salum Aboubakar 'Sure Boy'/Abdulhalim Humud, Ibrahim Mwaipopo/Abdi Kassim, Michael Kipre, John Bocco/Mwaikimba, Kipre Tchetche na Mrisho Ngassa.