Azam FC leo itajaribu kuvunja rekodi yake ya idadi ya pointi kwenye ligi kuu ya Vodacom itakapokwaana na Yanga katika uwanja wa taifa Dar es Salaam.

Rekodi ya juu ya pointi kwa Azam FC ni 40 ilizopata msimu uliopita lakini leo endapo itashinda itakuwa katika nafasi ya kufikisha pointi 41 na hivyo kuvuka idadi ya juu ya pointi.

Kwa hiyo wakati mashabiki wengi wa Azam FC na Yanga wanaangalia mchezo wa leo kama wa Azam FC kuendeleza rekodi ya kuifunga Yanga baada ya kuifunga mara tatu mfululizo bila yanga kupata goli na endapo leo itashinda basi itakuwa ni mara ya nne mfululizo baada ya kuifunga 1-0 kweli ligi raundi ya kwanza, 2-0 mechi ya hisani, 3-0 Mapinduzi Cup, Kuna rekodi nyingine muhimu ya idadi ya jumla ya pointi kwa Azam FC ambayo leo itakuwa ikitafutwa.

Wakati huo huo gazeti la mwananchi jana lililipoti kuwa KOCHA wa Azam, Stewart Hall amesema sababu kuu inayoathiri kiwango cha mshambuliaji wake John Boko anapokuwa katika kikosi cha Taifa Stars ni mashabiki wa Tanzania.Hall, raia wa Uingereza alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akijibu swali la mwandishi wa Mwananchi aliyetaka kufahamu sababu inayosababisha mshambuliaji huyo kukosa umahiri wa kupachika mabao awapo katika kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' huku akionekana kuwa hatari anapoichezea klabu yake ya Azam.

Juzi Boko alizamisha mabao mawili kati ya matatu yaliyoipa Azam ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal huku pia akiendelea kushikilia ukinara wa ufungaji akiwa tayari amepachika mabao 13 kwenye ligi huyo inayoendelea. "Unajua Boko kwangu ni kama dhahabu kwa sababu tangu  amekuwa chini yangu ameshafunga mabao 28 kwenye mechi mbalimbali za ushindani kuanzia msimu uliopita hadi sasa,"alisema Hall.Alisema,"Tatizo ni moja tu, mazingira ya hapa na kule ni tofauti, kule kazi kubwa ya mashabiki ni kusubiri makosa yake ili wamlaumu, lakini hapa anapokosea huwa anasaidiwa, kule hakuna wa kumsaidia hilo ndio tatizo kubwa."

"Hii ni tabia mbaya sana ambayo mashabiki wa Tanzania wanatakiwa kubadilika ili soka hapa ipige hatua la sivyo itakuwa ni kulaumiana tu kila siku,

 kwa kweli hali hiyo imesababisha Boko apoteze kujiamini kwa sababu anajua akikosea tu atapigiwa kelele,"alisema Hall.

Aliongeza kuwa mbali ya kuathiriwa na kelele za kumlaumu kutoka kwa mashabiki, kubadilika kwa mifumo ya uchezaji kati ya ule wa klabuni kwake na Taifa Stars inaweza kuwa kikwazo kwa nyota huyo katika kufunga mabao.

"Lakini pia kuna utofauti wa mifumo, mimi hapa kuna namna ambavyo huwa nawapanga pale mbele, lakini kocha Jan Poulsen labda ana utaratibu wake mwingine ambao unaweza ukawa unamsumbua, vitu kama hivi huwa vinatokea na ndio maana hata Messi (Lionel) huwa hafanya hizuri akiwa na Argentina.