Timu bora hupata matokeo bora,  kauli hiyo imedhihirishwa leo baada ya Azam FC kuifunga Coastal Union 3-0 katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa uwanja wa Azam Chamazi jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo kwa Azam FC imefikisha pointi 38 katika msimamo wa ligi kuu ya Vodacom huku mshambuliaji John Bocco akiendelea kuongoza wafungaji kwa kufikisha jumla ya magoli 13 baada ya leo kufunga mara mbili.

Magoli hayo matatu yamevunja rekodi ya Coastal Union iliyoshinda michezo mitano mfulilizo na kuibakisha timu hiyo ikiwa na pointi zake 26.

Mchezo huo uliokuwa wa kasi katika vipindi vyote Bocco alifungua kalamu ya magoli katika dakika ya 10 baada ya kumalizia kazi nzuri ya Mrisho Ngassa.

Goli hilo liliongeza kasi kwa Azam na kutengeneza mashambulizi kadhaa huku wachezaji wake wakicheza kiwango cha juu na kuwaacha Coastal Union wakiwa na wakati mgumu.

Dakika ya 24 Kiungo Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ aliyekuwa nyota wa mchezo huo alitengeneza pasi ya mwisho kwa Bocco aliyeweka mpiwa wavuni na kuandika goli la pili kwa Azam FC.

Sure Boy aliendelea kulinyanyasa lango la Coastal Union baada  ya kupiga shuti lililogonga mwamba na kurejea uwanjani, Azam  walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa 2-0 dhidi ya Coastal Union.

Kipindi cha pili kilianza Coastal walifanya mabadiliko mawili kwa wakati mmoja, walitoka Ramadhani Wasson na Francis Busungu nafasi zao zikachukuliwa na Ally Ahmed ‘Shiboli’ na Laurent Mgai mabadiliko ambayo yaliongeza kasi na kutengeneza mashambulizi kwa Coastal.

Uzembe wa kipa wa Coastal Union Godson Mmasa kuacha lango wazi liliwapa nafasi Azam FC kufunga goli la tatu kupitia kwa Kipre Tchetche aliyeachia shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.

Coastal watajutia nafasi walizopata dakika ya 55 na dk 86 wakati wachezaji Rashid Mandawa na Ally Ahmed walioshindwa kuipatia angalau goli la kufutia machozi timu hiyo baada ya kupiga mipira iliyookolewa na kipa Mwadin Ally wa Azam FC.

Azam walifanya mabadiliko dk 59 alitoka Ibrahim Mwaipopo akaingia Abdi Kassim, dk 71 Michael Kipre baada ya kuumia goti nafasi yake ikachukuliwa na Jabir Azizi na dk 75 aliingia Gaudence Mwaikimba kuchukua nafasi ya John Bocco.

Azam FC, Mwadini Ally, Waziri Salum, Said Morad, Aggrey Moris, Michael Kipre/Jabir Aziz, Kipre Tchetche, Ibrahim Mwaipopo/Abdi Kassim, John Bocco/Gaudence Mwaikimba, Salum Aboubakar na Mrisho Ngassa.