Kiungo Abdi Kassim Babi leo alifunga goli lake la kwanza akiwa na Azam FC lakini akatengeneza mengine mawili na kuisaidia Azam FC kuchapa JKT Oljoro 3-0 katka mchezo mkali wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa kwenye uwanja wa Chamazi.

Kumradhi; taarifa hii ni ya jana lakini imechelewa kutoka kutokana na mtandao wa internet kusumbua.

Azam FC wamepata pointi hizo tatu muhimu na  kufikisha jumla ya pointi 32 chini ya Simba wanaoongoza kwa kuwa na pointi 34, na kuiacha Oljoro ikibaki na pointi zake 26.

Mchezo huo uliochezwa uwanja wa Azam FC, Azam wakiwa wenyeji waliitumia vyema nafasi ya uenyeji kwa kuweka rekodi tatu muhimu.

Rekosi ya Kwanza; Azam FC Azam FC imefikisha pointi 32 baada ya kushuka dimbani mara 16 ikiwa ni rekodi kwa Azam FC tangia ianzishwe, Pointi 32 ni ziada ya pointi tisa (9) walizozipata msimu wa kwanza baada ya kupanda daraja kwani Azam FC ilimaliza ligi ikiwa na pointi 23 msimu huo huku ikiepuka kutokushuka daraja. Ligi ilikuwa na michezo 22.

Pointi 32 ni pungufu kwa pointi mbili katika msimu uliofuatia wa 2009/2010 kwani Azam FC licha ya kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu lakini ilimaliza na pointi 34, pointi 20 Nyuma ya vinara wa ligi hiyo Simba ambao walimaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote wakiwa na pointi 54. Katika msimu huo pia Azam FC ilishuka dimbani mara 22.

Katika msimu uliopita  wa 2010/2011, Azam FC ilimaliza msimu ikiwa na pointi 40, kwa hiyo hivi sasa Azam FC ipo nyuma kwa pointi nane (8) licha ya kucheza michezo 16 tuu, michezo sita nyuma ya michezo ambayo Azam FC walicheza msimu uliopita uliokuwa na michezo 22.

Yote hii inaonesha kuwa kiwango cha Azam FC kimepanda mwaka hadi mwaka, Webmaster anawapongeza viongozi wote, benchi la ufundi na wachezaji kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuipaisha Azam FC.

Rekodi ya pili; Mshambuliaji John Raphael Bocco anaongoza mbio za kusaka kiatu cha dhahabu akiwa amefunga magoli 11 katika mechi 16. Msimu wa 2009/10 kiatu cha dhahabu kilienda kwa Mussa Hassan Mgosi baada ya kufunga magoli 14, Bocco alimaliza na magoli 12, idadi ambayo alimaliza nayo mwaka jana ambapo kiatu cha dhahabu kilitwaliwa na Mrisho Ngasa.

Magoli 11 katika mechi 16 huku kukiwana na mechi 10 mkononi msimu huu kunatoa picha kwamba Bocco anaweza kuvunja rekodi yake na ya VPL ambayo inashikiliwa na Boniface Ambani na Mohammed Husein Mmachinga wote kutoka Yanga ambao waliwahi kufunga magoli 18 msimu mmoja. Tusubiri tuone kitakachojiri May 6, 2012. Wakati pazia la msimu wa 2011/12 litakapofungwa.

Rekodi ya Tatu; ni ya kufungwa magoli machache zaidi, Azam FC hadi sasa imeruhusu magoli sita tuu na kuweka rekodi ya msimu, Ligi Kuu na kwa klabu pia. Ukuta uliotengeneza rekodi hii ni Aggrey aliyecheza dakika 1430, Said Moradi aliyecheza dakika 1380, Erasto Nyoni aliyeshuka dimbani dk 1290, Waziri Salum 1296, Mwadini Ally 1170, Obren Curkovic dk 270, Ibrahim Shikanda 282, Haji Nuhu dk 44 na Luckson Kakolaki dk 16. Rekodi hizi zinawahusu wachezaji wa eneo la ulinzi na golikipa pekee.

Golikipa Mwadini Ally ambaye amefungwa magoli manne hadi hivi sasa naye amefikisha mechi ya tisa (9) pasipo kufungwa msimu huu.

Bocco alikuwa wa kwanza kufungua kalamu ya magoli kwa kufunga goli la kwanza dakika ya 23 kwa kichwa cha kinyumenyume akiunga mpira uliopigwa na Abdi Kassim.

Kabla Oljoro hawajakaa vizuri Azam walifanya mashambulizi dakika ya 27 Mrisho Ngassa aliongeza goli la pili akimalizia kazi nzuri ya Abdi, na kupeleka mapumziko Azam wakiwa mbele kwa 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi Oljoro wakibadili mchezo na kuanza kushambulia lakini dakika ya 54 Abdi aliifungia Azam goli la tatu akitumia vema uzembe wa beki wa Oljoro Yusuf Chikogote na kupiga shuti lililomshinda kipa wa Oljoro Said Lubawa na kutinga wavuni.

Goli hilo la tatu lilichanganya timu ya Oljoro wakianza kushambulia lakini hawakuweza kubadilisha matokeo hayo na kuifanya Azam ipate ushindi wa 3-0.

Azam FC kama kawaida viungo walianza kucheza kandanda lao la kawaida wakiongozwa na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Abdulhalim Humud na Jabir Aziz waliweza kuwasumbua wachezaji wa Oljoro.

Kipindi cha pili kocha Stewart Hall alimtoa John Bocco dk 65 akaingia Gaudence Mwaikimba, dk 68 aliingia Kipre Tchetche kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa na Luckson Kakolaki aliingia kuchukua nafasi ya Aggrey Morris.

Azam FC Mwadini Ally, Ibrahim Shikanda, Waziri Salum, Aggrey Morris/Luckson Kakolaki, Said Morad, Abdulhalim Humud, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Abdi Kassim, John Bocco/Gaudence Mwaikimba, Mrisho Ngassa/Kipre Tchetche na Jabir Aziz.