Timu ya Azam FC imeanza vizuri mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom kwa kuifunga African Lyon 2-1 katika mchezo uliochezwa leo jioni kwenye uwanja wa Azam FC, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Azam FC wakiwa wageni wa Lyon lakini kwenye uwanja wa nyumbani wa Azam FC, walipata pointi tatu muhimu na kurejea katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu kwa kufikisha pointi 26.

Katika mchezo huo ambao Azam FC imelipiza kisasi kwa kuifunga timu hiyo ambayo katika mzunguko wa kwanza Lyon waliifunga Azam 1-0 mchezo uliochezwa uwanja huo huo.

Azam FC katika mchezo huo walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 16 baada ya beki wa Lyon Hassan Mwamba kujifunga wakati akiokoa mpira wa Aggrey Morris wa Azam FC, na kuipatia Azam goli la kwanza.

Mpira ulibadilika na kuongezeka kasi  kwa dakika tano ambapo mchezaji wa Lyon, Semmy Kessy aliisawazishia timu yake goli hilo baada ya mabeki wa Azam utokuwa makini.

Kupatikana kwa goli hilo kuliamsha kasi ya mashambulizi kwa Azam FC ambapo dakika ya 26 John Bocco alikosa kuifungia timu yake na kupiga nje kama ilivyokuwa kwa Mrisho Ngassa aliyekosa nafasi tatu za wazi.

Dakika ya 36 mpira wa kichwa uliopigwa na Bocco uliandika goli la ushindi kwa Azam FC baada ya kutumia vyema mpira wa kona iliyopigwa na Abdi Kassim.

Goli la Bocco limemuongezea idadi na kufikisha jumla ya magoli 9 aliyofunga kwenye ligi kuu sawa na Kenneth Asamoah wa Yanga.

Kipindi cha pili timu zote zilirudi zikiwa na matumaini ya kuongeza magoli hayo Azam FC walifanya mabadiliko dk 53 waliingia Gaudence Mwaikimba na Ibrahim Mwaipopo kuchukua nafasi za John Bocco na Jabir Aziz na dakika ya 79 alitoka Tchetche Kipre nafasi yake kuchukuliwa na Abdulhalim Humud.

Mabadiliko hayo yalibadili mchezo kwa Azam ambao walitumia muda mwingi kulinda lango lao kwa kuudhibiti mpira, katika vipindi vyote, Azam walionekana kuutawala mchezo hasa nafasi ya kiungo iliyokuwa chini ya Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Abdi Kassim ‘Babi’ na Jabir Aziz.

Azam FC itashuka dimbani siku ya Jumapili ya Januari 29 kucheza na Moro United, mchezo utakaochezwa kwenye uwanja huo huo.

Azam FC, Mwadini Ally, Waziri Salum, Aggre Moris, Erasto Nyoni, Said Morad, Sure Boy, Jabir Aziz/Ibrahim Mwaipopo, Abdi Kassim, Mrisho Ngassa, John Bocco/ Gaudence Mwaikimba na Tchetche Kipre/Abdulhalim Humud.