Mabingwa wa kombe la Mapinduzi 2012, Azam FC jana walipata mapokezi makubwa baada ya kurejea jijini Dar es Salaam wakitokea visiwani Zanzibar.

 

Katika mapokezi hayo yaliyoongozwa na Mkurugenzi na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Abubakari Bakhresa aliyekuja kupokea kombe hilo kutoka kwa wachezaji wake. Msururu wa magari, bendi ya matarumbeta na waandishi wa habari kibao walipamba eneo la Gati dogo la abiria wa boti Bandarini Dar es Salaam.

 

Abubakar aliyeonekana kuwa na furaha isiyo na kifani amewataka wachezaji hao kujituma na kuongeza juhudi kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kutwaa kombe la ligi kuu.

 

Timu hiyo imetwaa ubingwa baada ya kuifunga Jamhuri ya Pemba katika mchezo wa fainali uliochezwa Alhamis katika uwanja wa Amaan, Zanzibar.

 

Akipokea kombe hilo, Bakhresa amesema kombe hilo la kwanza limefungua njia ya kuleta makombe mengine ikiwemo la ligi kuu Tanzania bara.

 

Shamra shamra za mapokezi hayo yalianzia bandarini kuelekea katika makao makuu ya ofisi ndogo na kongwe za klabu hiyo yaliyopo zizima yalishuhudiwa na mamia ya watu, msafara wa timu ulikuwa na gari zisizopungua 15.

 

Wachezaji wakiwa hawajui kitu kinachoendelea walikuja kupokelewa na basi jipya aina ya Yutong ikiwa ni sehemu ya mapokezi yao kwa kuleta kombe hilo kubwa la kwanza katika klabu hiyo.

 

Mapokezi yalishuhudiwa na viongozi wa klabu, wafanyakazi wa kampuni ya Bakhresa, mashabiki waliojitokeza waandishi wa habari mbalimbali.

 

Wapiga matarumbeta walikuwa sehemu ya kufanya mapokezi hayo kupendeza na kuchezwa na kila mtu hasa wachezaji wa timu hiyo.

 

Visiwani Zanzibar, uongozi wa klabu ya Malindi FC iliwaandalia mabingwa hao tafrija fupi ya kuwapongeza kwa kutwaa ubingwa huo wa kombe la Mapinduzi iliofanyika jana mchana dakika chache kabla hawajaanza safari ya kurejea Dar. Ambako pia msafara wa matarumbeta uliwasindikiza wachezaji toka klabu ya malindi hadi bandarini Zanzibar