Timu ya Azam FC imetwaa ubingwa wake wa kwanza mkubwa baada ya kulitwaa kombe la Mapinduzi  2012 kwa kuwachabanga Jamhuri 3-1 katika mchezo wa fainali ya kombe hilo uliochezwa uwanja wa Amaan.

Azam FC wamefuta ndoto za Jamhuri za kutwaa kombe hilo na kukabidhiwa kiasi cha shilingi milioni tano na medali za dhahabu kwa kushusha kipigo hicho kilichiowaacha mashabiki wa timu hiyo kuondoka vichwa chini.

Safari ya Azam FC visiwani hapa imekuwa ya mafanikio kwa kupata kombe hilo linalofungua njia kwa makombe mengine.

Katika mchezo huo Azam FC  walicheza kandanda safi kama waliloonyesha katika mechi zilizopita wakati Jamhuri waliingia uwanjani muda wote walikuwa wanalinda lango lao lakini hawakuepuka kipigo hicho.

Jamhuri  walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 17 lilofungwa na Ally Othman Mmanga baada ya mabeki wa Azam na kipa mwadini kufanya uzembe na kushindwa kuokoa mpira huo.

Dakika ya 40 John Bocco alisawazisha goli hilo kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Jamhuri Jafari Talib na kupeleka timu hizo mapumziko zikiwa sare ya 1-1.

Kipindi cha pili Azam FC walikuwa makini zaidi kutafuta ushindi huo kwa kucheza mpira wa hali ya juu, Azam FC walipata nafasi ya kutawala mchezo nyakati zote kutokana na Jamhuri kucheza upande mmoja wa kuzuia.

Kiungo wa Azam Salum Aboubakari ‘Sure Boy’ aliwasumbua viungo wa Jamhuri akishirikiana na viungo wengine, Abdulhalim Humud, Abdi Kassim na Michael Kipre waliweza kutumia nafasi zao kutengeneza  mashambulizi mengi.

Dakika ya 87 beki wa Jamhuri Mrisho Ahmed alijifunga akiwa katika jitihada za kuokoa mpira wa kona uliopigwa na Mrisho Ngassa.

Ngassa aliyeingia kuchukua nafasi ya Abdi Kassim ‘Babi’ aliandika goli la tatu kwa Azam baada ya kumalizia kazi nzuri iliyotengenezwa na Kipre Tchetche ikamkuta Gaudence Mwaikimba na kutua miguu kwa Ngassa.

Ushindi huo wa 3-1 umeacha simanzi kwa Jamhuri na wazanzibari wengi umepeleka kombe hilo la kwanza kwa Azam FC tangu ilipoingia ligi kuu misimu minne iliyopita.

Golikipa Mwadini Ally amechaguliwa kuwa golikipa bora wa michuano hiyo kwa kufungwa magoli matatu tangu kuanza kwa michuano na mshambuliaji John Bocco ameibuka mfungaji bora kwa kuwa na magoli manne sawa na Ally Mmanga wa Jamhuri wote wamekabidhiwa zawadi na kiasi cha shilingi laki moja.