Azam FC kesho itashuka katika uwanja wa Amaan kukwaana na timu ya Jamhuri ya Pemba katika mechi ya Fainali ya michuona ya Mapinduzi Cup. Mechi ya kesho itaanza saa mbili na nusu usiku.

Katika mazoezi ya leo asubuhi, kikosi cha Azam FC kilionekana kuwa na ari nzuri ya mchezo na vijana wameahidi kufanya kila liwezekanalo kupata ushindi.

Taarifa ya mchezo wa nusu fainali kati ya Azam FC na Simba

“Kweli mpira hauna mwenyewe” yalikuwa ni maneno ya mashabiki walishuhudia Azam FC ikimvua ubingwa SC kwa kumfunga 2-0 katika mchezo wa nusu fainali ya kuwania kombe la Mapinduzi 2012 mechi hii ilifanyika jumatatu jioni tarehe 9/1/2012.

Baadhi ya mashabiki lukuki walibaki wakiwa hawaamini kilichotokea baada ya kumalizika kwa mchezo kwa Azam FC kuwafunga mabingwa hao watetezi 2-0.

Katika mchezo huo uliokuwa na kila aina ya kukamia na wachezaji kuumizana, Azam FC walipata goli la kwanza  mapema katika dakika ya saba kupitia kwa mshambuliaji mahiri John Bocco aliyetumia uzembe wa beki za Simba na kuachia shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja wa Simba.

Kupatikana kwa goli hili kulifanya mchezo huo kuwa mgumu kwa Simba na wachezaji wake wakaanza kucheza kwa nguvu zaidi ili kubadilisha matokeo hayo lakini haikuwezekana hadi mapumziko Azam FC walikuwa wakiongoza 1-0.

Kipindi cha pili kilianza Simba walifanya mabadiliko akitoka Uhuru Seleman nafasi yake kuchukuliwa na Salum Machaku, kuingia kwa mchezaji huyo hakukubadilisha matokeo zaidi ya kubadili mchezo na kumuumiza mchezaji Michael Kipre ambaye ilikuwa akitengeneza mashambulizi mengi.

Michael alitoka nafasi yake ikachukuliwa vyema na kiungo mkabaji mwenye uwezo mkubwa wa kutembea uwanjani na kuendesha timu Jabir Aziz.

Azam walifanya mabadiliko walitoka Abdi Kassim katika dk 78 wakati wote Abdi alikuwa anatengeneza nafasi na kujaribu kufanya mashambulizi ya kushtukiza, nafasi yake ikachukuliwa na Mrisho Ngassa, kuingia kwa Ngassa kulifanya Simba ipoteze matumaini ya kupata goli la kusawazisha.

Dk ya 84 alitoka mshambuliaji Kipre Tchetche  mwenye kasi akaingia Gaudence Mwaikimba aliyemaliza mechi hiyo kwa kufunga pili katika dakika za nyongeza (90+4).

Mwaikimba aliweza kumpiga tobo kipa wa Simba Juma Kaseja na kumfanya kipa huyo kupiga magoti asijue la kufanya, na kumaliza mpira Azam FC 2-0.

Katika mchezo huo viungo wa Azam FC waliokuwa wakiongozwa na Salum Aboubakar 'Sure Boy' walicheza mpira katika kiwango cha juu na kuweza kutengeneza nafasi nyingi katika vipindi vyote vya mchezo

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema ushindi huo ni sehemu ya kusaka kombe hilo, amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake.

“tumeshinda nusu fainali Simba ilikuwa ikitupa wakati mgumu lakini sasa tutafanya maandalizi zaidi ili kupata ushindi katika mchezo wa fainali” alisema kocha Stewart.

Azam FC kikosi kazi Mwadini Ally, Wazir Salum, Aggrey Moris, Erasto Nyoni, Said Morad, Abdulhalim Humud, Michael Kipre/Jabir Aziz, Salum Aboubakar, John Bocco, Abdi Kassim/Mrisho Ngasa na Kipre Tchetche/Gaudence Mwaikimba.

 

Simb. Juma Kaseja, Nassor Masoud/Shomari Kapome, Juma Jabu, Kelvin Yondan, Victor Costa, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Mutesa Mafisango, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’, na Uhuru Seleman/Salum Machaku.