Azam FC imeendeleza ushindi dhidi ya klabu ya Yanga kwa kuifunga 3-0 na kupata nafasi kuingia nusu fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup. Kwa kufungwa 3-0 na Azam FC Yanga imeiaga michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Yanga kupokea kipigo kutoka kwa Azam FC katika michezo tofauti tofauti msimu huu, Azam Fc iliiifunga Yanga kwenye ligi kuu 0-1 kabla ya kuichapa 0-2 kwenye mechi ya kirafiki ya hisani wiki mbili zilizopita na jana ikaisasambua 0-3 na hivyo kuifanya Yanga yenye nyota kama Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza na Kenny Asamoah kishindwa kupata japo goli moja huku Yew Berko akiruhusu magoli sita (6) toka kwa washambuliaji wa Azam FC.

Azam FC imefikisha pointi saba sawa na Mafunzo ambayo katika mchezo wake wa mwisho iliifunga Kikwajuni 1-0, Yanga na Kikwajuni wameaga michuano hiyo.

Katika mchezo huo Azam FC walipata goli la kwanza dakika ya 5 kupitia mkwaju wa penati iliyopigwa kiufundi na John Bocco baada ya Bocco kuangushwa akiwa katika nafasi ya kufunga.

Penati hiyo iliyoamuliwa na mwamuzi Ramadhani Kibo ilileta mtafaruku baina ya wachezaji wa Yanga na mwamuzi huyo na kama mwamuzi asingekuwa na busara basi baadhi ya wachezaji wa Yanga wangepata kadi.

Wakicheza mpira wa kiwango cha juu hasa sehemu za kiungo na washambuliaji Azam FC ikitumia kasi ya wachezaji wake wa pembeni mapacha wawili toka Ivory Coast, dakika ya 29 Kipre Tchetche aliifungia Azam goli la pili kwa shuti lililomshinda kipa namba moja wa Yanga Yaw Berko. Goli la Kipre lilikuwa tamu na lilionyesha ufundi wa hali ya juu alionao mshambuliaji huyu mfupi mwenye uwezo mkubwa wa kufunga

Yanga wakiwa na kikosi chao kamili kilichotua visiwani hapa kwa ajili ya mchezo huo kilikuwa na wakati mgumu wa kusawazisha magoli hayo kwa kuwa safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya kipa Mwadini Ally, Agrey Moris, Said Morad, WaziriSalum na Erasto Nyoni  ilikuwa imara muda wote wa mchezo. Lakini aliyetia fora hapo jana alikuwa kiungo Abdulhalim Humud ambaye alifanya kazi kubwa kuhakikisha kiungo cha yanga chini ya Niyonzima hawapati nafasi ya kucheza. Hakika Niyonzima hatamsahau Humud.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Azam FC wakiwa mbele kwa  mabao 2-0 dhidi ya Yanga, Kipindi cha pili kilianza timu zilirudi na kasi mara mbili, Yanga wakitaka kusawazisha ili kuvuka hatua hiyo Azam wao waliimarisha ulinzi kuhakikisha wanaingia hatua ya nusu fainali.

Ilikuwa ni dakika ya 59, Tchetche alipigilia msumari wa moto kwa Yanga baada ya kuipatia timu yake ya Azam goli la tatu akiunga mpira wa kichwa uliopigwa na pacha wake Michael Kipre.

Mpira wa goli hili ulianza kwa Tchetche Mwenyewe ambaye aliwapiga cheza walinzi kama watatu wa Yanga na kupiga krosi ambayo iliunganishwa na Abdi Kassim na mpira kwenda pembeni kwa Kipre Michael ambaye alionekana kujua aina ya mipira ambayo pacha wake Kipre Bolou alikuwa akihitaji

Goli hilo tamu (diving header) ni moja kati ya magoli mazuri lilipoteza ndoto za Yanga za kutaka kulipa kisasi kwa kuifunga timu hiyo, Yanga walibadili mchezo na kuanza kucheza kwa nguvu zaidi hali iliyopelekea wachezaji wa Azam kuchezewa rafu za mara kwa mara. John Bocco alilazimika kutoka baada ya kuchezewa rafu mbaya na Canavaro ambaye wiki mbili zilizopita alimchezea rafu mbaya Mrisho Ngasa na kumfanya akae nje katika mechi ya jana.

Yanga walifanya mabadiliko alitoka kipa anayeaminiwa Berko na kuingia Shaaban Kado, walitoka Kisambale na Nurdin Bakari wakaingia Hamis Kiiza na Omega Seme lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuwaokoa na kichapo.Azam FC ilipata pengo baada ya mshambuliaji wake hatari John Bocco kuumia katika dakika ya 64 na nafasi yake kuchukuliwa na Gaudence Mwaikimba, walitoka Tchetche na Abdi Kassim baada ya kufana kazi nzuri nafasi zao zikachukuliwa na Ibrahim Mwaipopo na Jabir Azizi walioongeza kasi ya mchezo na kumaliza mchezo huo Azam wakiwa washindi kwa 3-0.

Azam FC inasubiri kucheza na mshindi wa pili wa kundi B ambao wanamaliza hatua ya makundi kesho usiku, itacheza nusu fainali ya kwanza siku ya Jumatatu usiku katika uwanja huo.

Azam waliorudisha Yanga Dar, Mwadini Ally, Agrey Moris, Erasto Nyoni, Said Morad, Wazir Salum, Salum Aboubakar, Michael Kipre, Abdi Kassim/Jabir Aziz 69’, Abdulhalim Humud, John Bocco/Mwaikimba 64’  na Kipre Tchetche/ Ibrahim Mwaipopo 79’.

Yanga Yaw Berko/Kado, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir haroub, Bakar Mbegu, , Salum Telela, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Keneth Asamoah, Pius Kisambale/Kiiza na Kigi Makasi.